Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist ndikilo amehitimisha ziara yake ya Awamu ya Kwanza ya uwekaji mawe ya msingi kwenye viwanda tarehe 27 Agosti 2019.
Akiwa kwenye ziara yake hiyo Mhandisi Ndikilo alianza kwa kuweka jiwe la Msingi kwenye kiwanda cha kuchakata Mhogo cha Tanzania Huafeng Agriculture Development Ltd kilichopo Mkuranga. Kiwanda hicho kinajegwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.1 na kinategemea kutoa ajira 100 za moja kwa moja, katika awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuchakata Tan 200 za muhogo kwa siku.
Pia amewataka wakazi wa Mkuranga kulima muhogo kwani soko lipo la uhakika na ametoa rai kwa maafisa kilimo wote Mkoani humo kutembelea kiwanda hicho na kuhamasisha wananchi kulima muhogo. Aidha ameelekeza Sekretariet ya Mkoa wa Pwani kuandaa na kuitisha Mkutano wa wadau wa Muhogo Mkoa wa Pwani utakao lenga kujadiliana utaratibu mzuri wa kuuza na kununua muhogo. Vilevile ametoa wito kwa wakulima wote kukitumia Kituo cha utafiti wa kilimo kibaha ili kupata mbegu bora za muhogo.
Katika hatua nyingine ameweka Jiwe la Msingi kwenye Kiwanda cha kuchakata Betri Wilayani Rufiji.
Akipokewa na wakazi wa nyamwage wilayani Rufiji Mhe Ndikilo amewaeleza kuwa kuwepo kwa kiwanda hicho kunakwenda kuinua Uchumi wa Rufiji, kwani kitatoa ajira na kulipa mapato kwa Serikali. Aidha mwekezaji ataisaidia jamii kutatua changamoto mbali mbali.
Amewataka Uongozi wa Rufiji kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kuwa uwekezaji mkubwa wa Viwanda utakuwa katika ukanda huo kwa sababu ya uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika kutoka katika bwawa la Nyerere.
Afkifungua kiwanda cha Maziwa cha mothers diary kilichopo Ikwiriri, Mhe. Ndikilo amewataka wafugaji kufuga kisasa, kuchanja mifugo yao, kuandaa malisho na kuanzisha vyama vya wafugaji wa n'gombe wa maziwa.
Mhe. Ndikilo amehitimisha ziara yake ya uwekaji mawe ya Msingi kwenye Viwanda Awamu ya Kwanza kwa kuweka Mawe ya Msingi kwenye viwanda 15 katika Wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga na Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.