Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo,amepokea msaada wa mifuko 300 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni nne kutoka katika kampuni ya uzalishaji wa saruji ya Kisarawe Cement iliyopo katika Wilaya ya Kisarawe Mkoani humu.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika mwanzoni mwa wiki hii jana katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo huku likishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo katibu tawala wa Mkoa bibi Theresia Mmbando na wataalam wengine kutoka sekretarieti yaMkoa Pwani.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo mkurugenzi mkazi wa kampuni hiyo Samir Jaffar,alisema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa katika kukarabati kiwanja cha kufanyia maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayotarajiwa kufanyika mwisho mwa Oktoba mwaka huu.
Jaffar,alisema kuwa katika awamu ya kwanza wameamua kuchangia mifuko 300 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni nne na kwamba msaada huo utaendelea kutolewa kadri ya mahitaji huku akiomba ushirikiano na Serikali katika kuhakikisha bidhaa zao zinapata masoko ya uhakika.
"kampuni yetu inatambua mchango wa mkuu wa Mkoa katika jitihada za kuinua sekta ya viwanda mkoani kwetu lakini na sisi tupo tayari kuungana na mkuu huyu pamoja na Rais Dkt.John Magufuli kwa harakati ya kuwa na Tanzania ya viwanda hivyo tutaendelea kuchangia katika masuala yote ya maendeleo,"alisema Jaffar
Aidha,Jaffar alisema kuwa kwasasa kiwanda chao kinazalisha tani 300 na hii inatokana na kuwepo kwa miundombinu ya barabara ya kusafirisha bidhaa hiyo kuwa mibovu kwani kwasasa barabara wanayolazimika kuitumia kutoka Kisarawe kupitia Kiluvya inatakiwa gari libebe chini ya tani 10 jambo ambalo linakwamisha uzalishaji.
Alisema ,kwasasa uwezo wao ni kuzalisha tani 500 lakini hatahivyo wanashindwa kutokana na changamoto hiyo lakini kama miundombinu itakuwa sawa ni wazi kuwa wataweza kuzalisha zaidi na kwamba malengo yake makubwa ni kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha tani elfu kumi na kuendelea ambapo aliomba Serikali kunagalia namna ya kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo,aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo huku akisema saruji hiyo itatumika katika kukarabati uwanja wa maonyesho ya bidhaa za viwandani uliopo Picha ya Ndege Kibaha ambapo kukamilika kwa uwanja huo utasaidia kufanyika kwa maonyesho hayo yanayotarajia kuanza Oktoba 29 mwaka huu.
“Mkoa wa Pwani umekuja na mikakati ya kufanya maonyesho hayo kila mwaka ambapo kwa mwaka huu mkoa unamahitaji makubwa katika kukarabati uwanja huo na kwamba anaimani baada ya kukamilika kwa uwanja huo wazalishaji wa bidhaa za viwandani watapata fursa ya kutangaza bidhaa zao kupitia maonyesho hayo” alisema Mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia changamoto za barabara zilizotolewa na wamiliki wa kiwanda Kisarawe Cement,alisema kuwa Mkoa unajipanga kukabiliana na changamoto hiyo ili kuweza kutoa fursa kwa wawekezaji hao kupata unafuu wa kusafirisha bidhaa zao na hivyo kupanua wigo wa kiuchumi kwa wananchi na hata wawekezaji hao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.