Serikali Mkoani Pwani ,imeridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyo chini ya DAWASA ,pamoja na mkakati wake wa kufikisha maji safi na salama maeneo ya viwanda ikiwemo mradi wa maji Chalinze -Mboga utakaotumia bilioni 17.1 pamoja na mradi wa Soga kuelekea kiwanda cha nyama TANCHOICE utakaogharimu bilioni 1.1 .
Licha ya kuridhishwa na kasi ya utendaji kazi huo,imemuelekeza mkandarasi Shanxi co.ltd wa mradi wa maji Chalinze -Mboga hadi Msoga kuhakikisha anamaliza ujenzi huo kwa wakati ifikapo mwezi June mwaka huu ili kuondoa kilio cha wanaChalinze ambacho kimedumu kwa miaka mingi.
Akitoa rai hiyo, wakati wa kutembelea miradi hiyo ,Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alisema mradi ambao chanzo chake ni kutoka Ruvu Juu-Chalinze -Mboga umefikia asilimia 52 hivyo kasi iongezwe ili ukamilike kwa wakati lengwa.
Pamoja na hilo,alitembelea eneo la viwanda unapotekelezwa mradi wa maji Zegereni ambapo imeidhinishwa kiasi cha sh.bilioni 2.3 ambapo unatarajiwa kuanza mwezi June hivyo aliiomba DAWASA kuuchukulia uzito ili fedha ikitoka mradi uanze mara moja.
Alisema, mradi huu utanufaisha viwanda takriban 25 kwenye eneo hilo kwani halmashauri ya Mji wa Kibaha imetenga eneo hilo kwa ajili ya viwanda.
“Nikuombe mtendaji mkuu DAWASA ,mradi huu wa Zegereni ni muhimu sana, mkoa wa Pwani ni ukanda wa uwekezaji na viwanda hususan eneo hili, hivyo basi endapo taasisi wezeshe mtashirikiana kikamilifu na wawekezaji kuondoa kero ya maji,umeme na kuboresha barabara kwa hakika viwanda vitanufaika na kuzalisha hatimae kuingiza pato kwa serikali “
“Taasisi wezeshi ndio nguzo ,kama kuna kuwa na vikwazo ,wawekezaji hawa hawawezi kuanzisha uwekezaji na kuzalisha kwani nao wanahitaji faida na manufaa,”
Hata hivyo alielezea,kiwanda cha TANCHOICE ni kikubwa kwa Afrika Mashariki na kati ,uzalishaji utaanza wakati wowote ameitaka taasisi hiyo kumalizia hatua za mwisho za mradi Soga eneo la Kongowe ili mwekezaji aanze uzalishaji.
Nae mtendaji mkuu wa DAWASA Cyprian Luhemeja alisema ,wamejikita kutatua kero ya maji kwenye viwanda kwa kufikisha huduma hiyo kupitia miradi yake ambayo pia inakwenda kujibu kilio cha wananchi.
Alifafanua ,serikali imejipanga kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji na DAWASA inaunga mkono juhudi hizo kwa kusogeza huduma ya maji kwa wawekezaji hao.
Luhemeja alibainisha, mradi wa Soga umekamilika ,wapo katika hatua ya nzuri na utakuwa na uwezo wa ujazo wa lita milioni mbili kwa siku ,”na kuongeza Kiwanda cha TANCHOICE kijipange kwa kuwa maji ni mengi labda washindwe wao.
Ofisa miradi wa TANCHOICE ,Boniventure Mtei alisema, maji yamefika kiwandani kilichobakia ni kuweka mita na kuanza uzalishaji april 15 mwaka huu.
Aliushukuru uongozi wa mkoa na DAWASA kwa ushirikiano wao na kusema wanatarajia kutoa ajira kwa wazawa na kusaidia wafugaji kuwapa soko la uhakika .
Kwa upande wake ,mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameipongeza serikali ya awamu ya Tano kwani kwasasa hata akisimama katika mikutano maswali ya kero ya maji yamepungua na alielezea kuwa, Chalinze kilio chao kikubwa ni maji lakini mradi wa Chalinze -Mboga na Chaliwasa chini ya DAWASA kero ya maji inakwenda kuwa historia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.