Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wadau wote wa korosho wenye uwezo Mkoani hapa kujenga maghala makubwa na ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhia korosho.
Wito huo ameutoa wakati akifungua kikao cha wadau wa korosho Mkoa wa Pwani kilichofanyika Wilayani Mkuranga.
Pia ametoa wito maalum kwa Chama cha Ushirika cha Mkoa CORECU kufanyia ukarabati wa maghala yao yaliyopo Kibiti ili yaweze kupewa leseni ili yaweze kutumika.
Aidha alisema kuwa mpaka sas,a Mkoa kwa kushirikiana na Bodi ya Leseni za maghala umekubaliana kusajili maghala mawili ya kuhifadhia korosho ambapo moja litakuwa Mwanambaya Wilayani Mkuranga ambalo lina uwezo wa kuhifadhi tani 15,000 na lingine lipo kwenye kiwanda cha zamani cha korosho (TANITA) amabalo lina uwezo wa kuhifadhi tani 5,000
Alifafanua zaidi kuwa ghala la Mwanambaya lililopo Mkuranga litapokea korosho kutoka wilaya za Mkuranga, Mafia, Kibiti na Rufiji na lile la TANITA litapokea korosho kutoka Kibaha, Kibaha Mji, Kisarawe, Bagamoyo na Chalinze.
“Natambua baadhi ya Wilaya zitakuwa mbali na maghala yaliyopatikana lakini kwa mujibu wa mfumo huu hilo siyo tatizo kwa kuwa gharama za usafirishaji zinawekwa kwenye mjengeko wa bei na si gharama ya moja kwa moja kwa chama cha msingi” alisema Ndikilo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu ambao wataonesha nia ya kutaka kujaribu au kuonesha nia ya kutaka kuhujumu mfumo huu wa stakabadhi ghalani kwani Serikali ya Mkoa haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.
Mhandisi Ndikilo aliongezea kwa kusema kuwa mfumo huu wa stakabadhi ghalani katika ukusanyaji na uuzaji wa zao la Korosho ni agizo la kitaifa.
Pia ameongeza kuwa mfumo huu unawawezesha wakulima kuwa na sauti moja katika katika kupigania haki yao kwenye biashara ya korosho ghafi dhidi ya walanguzi na madalali wao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.