“Hakuna Mwananchi yeyote atakayethubutu kuingia katika msitu huu na kufanya uharibifu,na msitu huu tutaulinda kwa maslahi mapana ya nchi”
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa mwishoni mwa wiki hii ambapo Mkoa uliadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti 2000 katika msitu wa Kazimzumbwi uliopo Wilayani Kisarawe
Aidha Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi kutunza misitu na kusisitiza kuwa serikali haitakuwa na mchezo kwa yeyote atakayebainika kuharibu misitu huo kwa kufanya shughuli za kibinadamu ikiwa pamoja uchomaji mkaa na kufyeka msitu.
Pia Mhandisi Ndikilo aliwataka wananchi kulinda misitu kwa faida yao wenyewe kwani misitu ina faida nyingi kwa binadamu na kuwa ikutunzwa vizuri bila kuvamiwa ni chanzo kikubwa cha hewa ya oxigeni lakini pia itasaidia kurekebisha mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akisoma risala katika maadhimisho hayo afisa mali asili Mkoa wa Pwani Felix Shayo alisema Mkoa wa Pwani una upungufu wa watumishi wa sekta ya maliasili 95 , hali iliyoelezwa kukwamisha juhudi za kuzuia uharibifu na utoroshaji wa mazao ya misitu.
Shayo alisema Ili kukadhibiti hali hayo ya uharibifu wa misitu Mkoa unahitaji jumla ya watumishi wa sekta hiyo wapatao 156 na waliopo ni 58.
Alisema uhaba wa watumishi hao umepelekea kukwamisha shughuli mbalimbali za misitu na hivyo misitu kuwa hatarini kuvamiwa na mazao yake kuchukuliwa kiholela.
Katika hatua nyingine , Shayo aliiomba serikali kuongeza watumishi hao Mkoani humo ili wasaidie kusimamia na kudhibiti rasilimali za misitu.
Aidha aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutumia nishati mbadala ili kuacha ama kupunguza matumizi ya mkaa ambao ndio chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu Mkoani humo
Kauli mbiu mwaka huu ni Tanzania ya Kijani inawezekana, Panda Miti kwa maendeleo ya Viwanda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.