Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wananchi Mkoani hapa kuacha mara moja tabia ya kuhifadhi wahamiaji haramu, na yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hayo ameyasema wakati alipofanya mkutano na Waandishi wa habari baada ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu 12 , Waethiophia 11 na msomali 1 pamoja na watanzania wawili ambao ni wasafirishaji .
Mhandisi Ndikilo amesema kuwa, wahamiaji hao walikamatwa baada ya Idara ya Uhamiaji Mkoani hapa kupata taarifa ya kintelejensia kutoka kwa raia mwema juu ya uwepo wa raia hao wa kigeni wakiwa wamejificha katika mapori ya ruvu darajani , ambapo Ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa ilifanya msako kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na kufanikiwa kuwatia mbaroni raia wahamiaji haramu hao 12 wakiwa wamejificha katika pori hilo.
“Natoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutupatia taarifa zenye tija, pale wanapowaona watu wasiowafahamu kwenye maeneo yao ili vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viweze kuchukua hatua haraka “alisema Mhandisi Ndikilo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ndikilo ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani hapa, kudhibiti maeneo yote ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahamiaji haramu kuingia ndani ya Mkoa wa Pwani na kuhakikisha wanadhibiti mtandao wa usafirishaji wa wahamiaji hao majini na nchi kavu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.