Serikali Mkoani Pwani, imetoa rai kwa Watendaji,Wenyeviti wa Mitaa/Vijiji na wataalam kuhakikisha wanashirikiana na wadadisi na wasimamizi watakaofanya kazi ya utafiti wa kilimo mwaka 2017/2018, ili kupata takwimu halisi.
Hatua hiyo itasaidia, kupanga mipango ya maendeleo katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watanzania hasa katika maeneo ya Vijijini.
Akifungua mafunzo ya siku tano ya wadadisi wa utafiti wa kilimo mwaka huu wa fedha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo, alisisitiza endapo utakuwepo ushirikiano mzuri utawezesha kuweka mikakati ya baadae ya Kimkoa na Taifa.
Aidha aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi na wasimamizi hao ili kutoa taarifa sahihi kuhusiana na utafiti.
Mhandisi Ndikilo, alieleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya takwimu namba 9 ya mwaka 2015 taarifa zitakazokusanywa zitatunzwa kwa usiri na zitatumika kusimamia kupatikana takwimu halisi za kilimo.
Aidha alisema kuwa, sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi ambapo mwaka 2016 mchango wa sekta hiyo pato la taifa ulikuwa asimilia 29.1,
”kati ya asilimia hiyo kilimo cha mazao kilichangia asilimia 15.5, Mifugo asilimia 7.7, misitu asilimia 3.9 na sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 2.0 “ alisema Mhandisi Ndikilo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa alisema kuwa, mafunzo hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mipango ya kuboresha maisha ya watanzania.
Mhandisi Ndikilo, alifafanua kuwa Serikali imeandaa mipango madhubuti ya muda mfupi na mrefu inayolenga katika kuimarisha uchumi na kuondoa umaskini ikiwa ni pamoja na dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025. Serikali na wadau bado inaendelea kuhitaji takwimu rasmi kwa ajili ya kupanga utekelezaji na kutathmini program mbalimbali za maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Mhandisi Ndikilo aliishukuru Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la mendeleo ya Kitaifa USAID kwa msaada wa kiufundi na fedha uliowezesha kufanikisha utafiti
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.