Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amekabidhi jumlaya vitambulisho 35,000 vya wafanyabiashara Ndogondogo (wamachinga) kwa Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Pwani kwa awamu ya pili.
Akikabidhi vitambulisho hivyo mwishoni mwa wiki hii, Mhandisi Ndikilo amewataka Wakuu hao wa Wilaya kulisimamia vizuri zoezi hilo la ugawaji wa Vitambulisho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, na kuhakikisha vinagawiwa kwa wafanya biashara ndogondogo wote katika Mkoa wa Pwani.
Pia amewataka kuwasimamia vizuri watendaji wa Halmashauri ili waweze kulitekeleza zoezi hili la ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa busara kubwa.
Aidha alisema kuwa ,kila Halmashauri ihakikishe inagawa vitambusho hivyo kwa wafanyabiashara wote na kusisitiza kuwa kila mfanyabiashara lazima awe na kitambulisho na hataruhusiwa kufanya biashara ya aina yeyote kama hatakuwa na kitambulisho hicho..
“Yeyote Yule anayefanya biashara na halipi kodi TRA wala hana mashine ya EFD basi huyo anapaswa kupewa kitambulisho hicho”Alisema Mhandisi Ndikilo.
Mkoa wa Pwani umepokea jumla ya vitambulisho 60,000 kwa awamu zote mbili,ikiwa ile ya kwanza Mkoa ulipokea vitambulisho 25,000, na awamu ya pili mkoa umepokea vitambulisho 35,000 ambapo vyote vimegawiwa katika Halmashauri zote tisa ambapo kila mfanyabiashara anayepaswa kupewa kitambulisho hicho atatakiwa kulipa elfu ishirini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.