Timu ya mpira wa miguu ya RS Pwani imeendelea kung’ara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya timu ya Halmashauri ya Mji Kibaha (Kibaha TC) katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Mei 1,2025 katika Uwanja wa Jeshi la Zimamoto, Kibaha mkoani Pwani.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Mhandisi Alphaxsady Msengi, ambaye pia ni nahodha wa RS Pwani, aliipatia timu yake bao la kwanza dakika ya 30 ya kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Kibaha TC walirejesha matumaini dakika ya 40 kwa kusawazisha bao hilo na kufanya matokeo kuwa 1–1 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambapo dakika ya 68 Elius Maige aliiongezea RS Pwani bao la pili na la ushindi, lililodumu hadi filimbi ya mwisho ya mchezo.
Akizungumza baada ya mchezo, Kocha wa RS Pwani, Bw. Emanuel Lugomolwa, alisema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri na nidhamu ya wachezaji wake. “Tumekuwa tukijitahidi kuandaa timu vizuri. Ushindi huu ni motisha kwa timu, na tunaendelea na mpango wa mechi zaidi za kirafiki ili kuongeza uimara wa wachezaji wetu,” alisema.
Kocha Lugomolwa pia alitoa wito kwa watumishi wengine kutoka ofisi yao kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo, akisisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya ya mwili na akili.
Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani sherehe zilifanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, chini ya ugeni rasmi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.