Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imekamata salfa ya wizi mifuko 247 yenye thamani ya Tshs 6,916,000 katika kijiji cha Msonga ikiwa katika maandalizi ya kuanza kuuzwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Filberto Sanga akizungumza mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na baadhi ya watendaji na wataalam mbalimbali alisema ”Siku ya alhamisi ya tarehe 3/08/2017 usiku walibaini kuna salfa nyumbani kwa mwananchi mmoja hivyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi salfa hizo zilikamatwa na kuhifadhiwa zikisubiri upelelezi ukamilike”.
Mhe. Sanga alisema kuwa baada ya upelelezi kukamilika salfa hizo zitagawiwa kwa wananchi wa Mkuranga kama salfa za awali zilivyogawiwa.
Aidha Mhe. Sanga ametoa wito kwa watendaji wote wa Serikali kuwa waaminifu na kuacha ubadhilifu na udanganyifu katika mali za umma.
Mhe. Sanga alisema Wilaya ya Mkuranga ilipokea pembejeo za ruzuku kwa asilimia mia moja za korosho, kiasi cha kilo 453,875 sawa na mifuko 18,155 ya salfa ya unga katika awamu 4, yaani mifuko 8,314, mifuko 5,998, mifuko 2,390 na mifuko 1200. Pia jumla ya lita 6,886 za salfa ya maji, lita 1,231 dawa za wadudu na mabomba 41.
Kupitia kamati ya pembejeo ya Wilaya, mgao wa pembejeo hizo ulifanyika kwa kila Kijiji kwa kutumia kigezo cha idadi ya mikorosho.
Mhe. Sanga alisema pamoja na mafanikio ya ugawaji wa pembejeo hizo kuna changamoto zilizojitokeza ikiwemo udanganyifu kwa upande wa wakulima kwa kutoa takwimu za uongo juu ya idadi ya mikorosho waliyonayo kwa lengo la kupatiwa mgao mkubwa wa pembejeo. Vilevile pembejeo kutotosheleza mahitaji halisi kwa wakulima kwani kuna upungufu wa takribani tani 346 za salfa ya unga, lita 7,000 za salfa ya maji, lita 3,000 za dawa za wadudu na mabomba 85. Pia changamoto kwa baadhi ya Watendaji wa Vijiji kutowasilisha takwimu za mikorosho kwa Vijiji vyao mfano Kijiji cha Marogoro kata ya Vianzi na kusababisha wakulima wa maeneo hayo kukosa pembejeo.
Akizungumza namna ya kutatua changamoto hizo Mhe. Sanga alisema mpaka sasa Wilaya imepeleka maombi ya kupatiwa nyongeza ya pembejeo na imefanikiwa kupatiwa tani 10 zaidi za salfa ya unga lakini pia Watendaji wameelimishwa juu ya ukusanyaji wa takwimu sahihi za mikorosho kutoka kwa wakulima japo takwimu hizi hazikuweza kutumika tena msimu huu bali zitatumika kwa msimu ujao.
Mhe. Sanga alisema wakulima wengi wamehamasika kusafisha mashamba yao hasa baada ya kuambiwa kigezo kimojawapo cha kupatiwa pembejeo ni kuwa na shamba la mikorosho lililopaliliwa, vilevile Wilaya imeweza kupata takwimu za awali za idadi ya mikorosho waliyonayo wakulima. Hii itasaidia kutathmini mahitaji halisi ya pembejeo.
Bi. Julita Bulali - Afisa kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Wilaya ya Mkuranga alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa takwimu sahihi kutokana na wakulima kutokuwa na ushirikiano, hivyo katika harakati za kupambana na changamoto hiyo viongozi wa Vijiji wakiwemo Wenyeviti wa Vitongoji wameagizwa kubainisha idadi ya mikorosho.
Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya zinazolima korosho na kwa Mkoa wa Pwani inaongoza kwa kuwa na takribani mikorosho milioni tatu na inazalisha wastani wa tani 9,000 kwa mwaka.
Katika msimu wa 2016/2017 wilaya imeuza korosho kiasi cha kilo 6,647,081 na kuingiza jumla ya Tshs 15,846,498,022.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.