Mwenyekiti wa kamati ya Usalama mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakari Kunenge amesema Serikali inaendelea kusimamia Maamuzi ya hukumu za mahakama katika migogoro ya ardhi kata ya Mapinga.
Amewashauri kuwa pande zote mbili ambazo ni walioshindwa na walioshinda mashauri yao kuona kama inafaa waketi meza moja ili kufanya maridhiano.
Akitoa msimamo wa Serikali na kamati iliyoundwa na Waziri wa ardhi Angelina Mabula kushughulikia migogoro iliyokithiri katika kata ya Mapinga, Kunenge amesema kuwa hawawezi kuipinga mahakama kutokana na maamuzi iliyoyafanya.
Akiwa kwenye utekelezaji eneo la Kiaraka, aliwaasa zaidi ya wananchi 250 wanaodaiwa kuingilia eneo halali la Balozi Saimon Mlai waondoke kama Maamuzi ya Mahakama Kuu ilivyoelekeza.
Ameeleza kuwa Mahakama ilituma dalali kufika kwenye eneo hilo na kuwaondoa wananchi wavamizi na kuwa eneo ni mali halali ya Balozi Mlai ambaye ndiye mwenye hati halali ambayo haijabatilishwa.
Katika eneo hilo, mwakilishi wa wananchi Jeremiah Mtema alisema kuwa wapo tayari kwa maridhiano kati yao na wenye eneo hilo ili maisha yaendelee.
Kufuatia kauli hiyo, Kunenge ametoa wiki kwa wananchi kuonana na mwenye eneo kuangalia namna ya kumaliza tatizo hilo lakini ambae hataki maridhiano aondoke kupisha eneo.
Vile vile Kunenge alifika kwenye eneo lenye mgogoro baina ya taasisi ya Kijiko na wananchi 15 wanaodaiwa kuvamia eneo hilo, ambapo amewataka wananchi waache kuendeleza chochote cha maendeleo na kwamba naye Kijiko asiwabughudhi wananchi hadi hapo Suluhu ya mahakama au maridhiano itakapokamilika.
"Katika mgogoro huu, hakuna mwenye haki hadi sasa, hivyo ushauri ni kwenda kufungua kesi ili haki itendeke, pia wanaweza kukaa meza moja ili kuweka maridhiano ambapo upande wa Serikali kutakuwa na watalaam ambao watasimamia, hatimae mgogoro huu uishe na kila mmoja aendelee na maendeleo yake," alisisitiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.