Serikali Mkoani Pwani ,imeelekeza wakulima na wafugaji watumie bonde la mto Ruvu kwa kuheshimiana na kufuata sheria pasipo kundi lolote kuwa kero ya mwingine ,na kusisitiza ni bonde muhimu kwa jamii zote hizo .
Aidha serikali Mkoani hapo imewaasa wakuu wa wilaya ,maafisa tarafa,wakurugenzi na wataalamu mbalimbali,kwenda kwa wananchi kujua changamoto na kero ambazo bado ni kilio kwao ili kuzitafutia ufumbufu badala ya kusubiri kupelekewa kero ofisini ama wananchi kuzifikisha ngazi za juu .
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ametoa rai hizo wakati alipofanya kikao cha kazi ,kujichimbia na Wakuu wa Wilaya kuweka Mikakati ya kutatua Kero za Wananchi, Migogoro ya Ardhi na kutathimini Miradi ya Maendeleo Mkoani humo .
Ameeleza ,serikali ya mkoa haijawahi kutamka jamii moja iondoke katika bonde hilo, bali inasisitiza kuishi kwa amani na kuheshimiana bila kuingiliana kwenye majukumu yao na kundi moja kulia kutokana na kundi jingine kumsababishia hasara .
Ndikilo amesema ,bonde hilo lina ardhi yenye rutuba,malisho na maji na inafaa kwa makundi yote .
Hata hivyo, amewataka wafugaji wenye mifugo mikubwa kwenda kuchukua vitalu Ranchi ya Ruvu kwa bei nafuu iliyopangwa ili kuondoa migogoro .
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa wa Pwani, anataka viongozi mbalimbali na wakuu wa wilaya na kata kusimamia miradi ya maendeleo ,na kuhakikisha inajengwa kwa wakati na kuzingatia viwango .
Kikao hicho pia kilihusisha kamati ya Usalama Mkoa na Wakuu wa Taasisi za Serikali Mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.