Serikali imeanza ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Kirongwe wilaya ya Mafia mkoani Pwani ili kuwaondolea wakazi wa kata hiyo adha ya kutembea zaidi kilometa nane kwenda kufuata matibabu katika hospitali ya Wilaya.
Akizungumza na kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi ya mkoa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Shaibu Nunduma amesema kituo hicho kinajengwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo katika awamu ya kwanza tayari serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji, jengo la wagonjwa wa ndani na nyumba za madaktari.
Naye mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia dokta Zuberi Mzige amesema ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika kitahudumia wananchi wa kata za Kanga, Kirongwe, Baleni na Ndagoni zenye vijiji 13 .
Mhe. Nunduma aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo pia kutapunguza idadi ya vifo vya akinamama wajawazito ambao walikuwa wakipoteza maisha wakati wa kusafirishwa kwenda kujifungulia katika hopitali ya wilaya.
Aidha aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili na nusu takwimu zilionesha kuwa akinama wajawazito tisa (9) walifariki dunia wakiwa njiani wakipelekwa hospitali ya Wilaya kujifungua.
Akizungumza Mara baada kutembelea ujenzi huo mwenyekiti CCM Mkoa wa Pwani Mhe. Ramadhani Maneno ameipongeza serikali kwa kujenga kituo hicho na kuitaka iharakishe kukamilisha ujenzi huo ili huduma zianze kutolewa mapema.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evaristi Ndikilo ameiagiza Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Mafia kuhakikisha inakamilisha mradi huo kabla ya mwezi Desemba mwaka huu kama ilivyokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.