Kamishna wa Sensa Tanzania Bara Anne Makinda,amewapiga marufuku baadhi ya wananchi na viongozi mbalimbali wanaohusisha suala la Sensa na mambo ya kisiasa kuwa waache maramoja.
Amesema ,Sensa inafanyika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa ambayo itasaidia Serikali kutoa huduma za kijamii kwa uhakika kulingana na idadi ya watu wake na kusema Sensa haina mahusiano na siasa.
Makinda,ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Muheza uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha Wananchi kujitokeza katika Sensa ya majaribio ya mwaka huu.
Amesema ,hataki kusikia mtu analeta siasa katika suala la Sensa na wala lisiwe suala la madhehebu ya dini na kusema Sensa ni suala la maendeleo la Taifa na wananchi wake na endapo mtu ataingiza siasa lazima sheria itachukua mkondo.
Makinda,amesema kuwa Sensa ya majaribio itafanyika Septemba 11 na kwa nchi nzima imepangwa kufanyika katika vituo 13 ikiwemo Mtaa wa Muheza Kibaha.
Amewataka wananchi hao waache kuleta ujanja wa kukwepa kuhesabiwa na badala yake wajitokeze kutoa ushirikiano kwa makalani wa Sensa na kutoa taarifa za ukweli kwa manufaa ya Taifa.
"Nimekuja hapa Muheza kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la Sensa ya majaribio itakayofanyika Septemba 10 kuamkia Septemba 11 ,kwahiyo nawaomba wote mjitokeze," alisema Makinda
Makinda,amesema Sensa itakayofanyika mwaka huu imeboreshwa zaidi na itafanyika kisasa kuanzia ngazi ya Kitongoji kwa hiyo ni wajibu wa kila mwananchi kutambua umuhimu wa Sensa .
Aidha ,Makinda amesema Sensa ya majaribio itawahusisha watu wote watakaolala usiku wa tarehe 10 kuamkia tarehe 11 Septemba na kila mtu atahesabiwa kulingana na maeneo aliyoamkia.
Makinda,ameongeza kuwa watakaohesabiwa mwaka huu katika Sensa ya majaribio na mwakani watahesabiwa kwakuwa lengo ni kupata takwimu sahihi na Sensa ya mwaka huu ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya mwaka 2022.
Kwa upande wake afisa wa Sensa Taifa Said Ameir,akiwa katika mkutano huo amesema wananchi wasiogope kuhesabiwa kwakuwa taarifa watakazozitoa ni siri na zitakwenda kutumika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na sio jambo lingine.
Ameir,amesema kuwa kama itabainika karani ametoa siri za mwananchi atachukuliwa hatua kwakuwa kitendo hicho kitakuwa ni cha uvunjifu wa maadili ya kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.