Timu ya michezo ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani imeshiriki katika uzinduzi wa Mashindano ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), yaliyofanyika leo, tarehe 07 Septemba 2025, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ambaye aliwataka washiriki wa mashindano hayo kuyachukulia kama fursa ya kujenga afya bora ili kuweza kutoa huduma nzuri na bora kwa wananchi.
Aidha, aliwataka viongozi wa SHIMIWI kuhakikisha kuwa wanaratibu mazoezi ya awali kwa wachezaji ili kuwaandaa kiakili na kimwili, pamoja na kuhakikisha upimaji wa afya unafanyika kwa kushirikiana na taasisi za afya nchini ili kupata wachezaji wenye afya bora na kuepuka matukio ya maradhi ya ghafla wakati wa mashindano.
Mhe. Dkt. Biteko alibainisha kuwa tasnia ya burudani, ambayo michezo ni sehemu yake, inaendelea kukua kwa kasi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa na kuongeza ajira. Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 sekta hiyo ilikua kwa asilimia 15, huku mwaka wa 2023/24 ikikua kwa asilimia 18.
Aliongeza kuwa watumishi wa umma nchini ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya michezo kupitia SHIMIWI, kwani wamekuwa wakikusanya maelfu ya wachezaji wanaoshindana na kuonyesha ari ya kimashindano, hivyo kuchochea jamii kuthamini michezo na kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, akitoa salamu za mkoa, aliishukuru Serikali kwa kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha michezo kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Kulea Vipaji katika Chuo cha Michezo Malya kwa zaidi ya shilingi bilioni 31.
Aidha, Mhe. Mtanda alitumia fursa hiyo kuwaalika tena SHIMIWI na mashirikisho mengine ya michezo kufanya mashindano yao mkoani Mwanza, akisisitiza kuwa mkoa huo una miundombinu rafiki ya viwanja, malazi, vivutio vya utalii, na maeneo safi ya kupumzika, hasa katika fukwe za Ziwa Victoria.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, alieleza kuwa mashindano hayo hayajawahi kusimama kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo. Aliahidi kuwa wizara itaendelea kuyasimamia kwa kuhakikisha yanakuwa ya haki na mshindi anapatikana kwa njia halali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.