Tume ya Utumishi wa Mahakama imetoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya katika Mkoa wa Pwani. Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo, kuongeza uelewa na ujuzi kwa viongozi na maafisa wa Mahakama waliopo kwenye kamati hizo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya maadili iliyopangwa.
Mafunzo hayo yamefanyika lFebruari 25,2025 Wilayani Kibaha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
Pamoja na mafunzo hayo, wajumbe hao walikula kiapo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Nickson Simon aliwataka wajumbe wa kamati hizo kuishi kwa kuzingatia kiapo chao na kufanya kazi kwa hofu ya Mungu, akisisitiza kuwa hofu ya Mungu ndiyo msingi mkuu wa maadili mema.
Nawasihi tuishi kulingana na kiapo chetu. Mkipokea malalamiko, muyafanyie kazi kwa kuzingatia misingi ya maadili na kuhakikisha tunakuwa wasimamizi wa maadili hayo. Msingi wa maadili yetu ni hofu ya Mungu,alisema Mhe. Nickson.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, aliwaasa wajumbe wa kamati hizo kufanya kazi kwa kuzingatia majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kupokea na kuchunguza malalamiko yanayowasilishwa na wananchi dhidi ya Mahakimu, pamoja na kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Mahakimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.