MHE. MKUU WA MKOA WA PWANI ATOA UFAFANUZI JUU YA MITA 120 ZA HIFADHI YA BARABARA YA MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist W. Ndikillo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Bibi Jenipher Omolo kuwashirikisha wananchi wa Mji wa Kibaha katika masuala yote ya maendeleo ya Mji huo.
Kauli hiyo aliitoa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Bwawani Mailimoja wakati akitoa ufafanuzi wa tafsiri ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro KM 16 kuanzia MBEZI - DAR ES SALAAM hadi KM 37 TAMCO - KIBAHA ambayo ilikuwa na utata ambapo wananchi walikuwa wakidai kutoshirikishwa.
Akifafanua suala hilo alisema kwamba hifadhi ya Barabara hiyo ya Morogoro (KM 16 kuanzia MBEZI - DAR ES SALAAM hadi KM 37 TAMCO – KIBAHA) ni Mita 120 ambapo kwa upande wa kulia ni Mita 60 na upande wa kushoto ni Mita 60 kutoka katikati ya barabara ambapo hapo awali ilikuwa ni Mita 240 ikiwa kushoto Mita 120 na kulia Mita 120, jambo ambalo lilizua malalamiko kwa wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa ilijadili suala hili kwa kina,na kuona kwamba zile Mita 240 za mwanzo zilikuwa kubwa sana hivyo ikamuandikia Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndipo likaja jibu kuwa upana wa hifadhi ya Barabara itakuwa ni Mita 120 tu na hakutakuwa na mabadiliko.
Pia Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwaambia wakazi na wafanyabiashara wa Mailimoja kuwa ile tarehe (23/11/2016) iliyoweka awali ya kubomoa nyumba zilizo kwenye hifadhi ya barabara hiyo ya Morogoro (KM 16 kuanzia MBEZI - DAR ES SALAAM hadi KM 37 TAMCO – KIBAHA) ameisitisha kutokana na wananchi kutojiandaa hivyo ameongeza muda wa miezi miwili hadi tarehe 23/01/2017 ili wananchi waweze kujiandaa na kuboamoa nyumba hizo.
Hata hivyo Mhe. Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kuanza mara moja ujenzi wa soko katika eneo la Loliondo, kabla ya ubomoaji wa soko la maili moja haujafanyika kwasababu ya eneo hilo la soko(Mailimoja) lipo ndani ya hifadhi ya Barabara.
Kwa upande wa Kituo cha Mabasi, ameeleza kwamba Kituo cha Mabasi cha Mailimoja kitabakia kuwa palepale mpaka Kituo kipya kilichoandaliwa kitakapomalizika kujengwa,na kuongezea kuwa Kituo hicho cha Mabasi kinachotumika sasa, kitatumika kwa mabasi makubwa yaendayo mikoani tu, na yale mabasi madogo ya kwenda Kongowe, Mlandizi, Chalinze, Morogoro, Msata na Mkata yatakwenda sehemu iliyoandaliwa (Loliondo) pamoja na magari ya mizigo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.