Utekelezaji wa kufundisha somo la kiingereza (English) kuanzia darasa la kwanza kufuatia mabadiliko ya mtaala wa elimu ya Msingi 2023 utaanza rasmi Januari, 2024.
Mwenyekiti wa Maandalizi ya mafunzo ya somo la Kiingereza (English) Prof.Gastor Mapunda, ameeleza hayo leo Novemba 20,2023 katika mafunzo kwa viongozi wa elimu Halmashauri ya Chalinze, Mkoani Pwani yaliyoandaliwa kwa kushirikiana baina ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ,Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania katika programu ya Mradi wa Shule Bora ambayo inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa Ufadhili wa Shirika la msaada la Uingereza (UKaid) na kwa usimamizi wa Cambridge Education.
Prof. Mapunda amewaasa walimu wa somo la kiingereza kuongeza umahiri wa kutosha ili kuleta matokeo chanya katika utekelezaji huo.
Amewataka maafisa elimu na wathibiti ubora wa shule kuyatambua maboresho hayo na kwenda kuyasimamia kikamilifu.
Awali mkuza Mtaala wa somo la Kiingereza kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET ), Neema Matingo alieleza mafunzo hayo yanalenga kuwapa uelewa mpana viongozi wa elimu kuhusu mabadiliko ya mtaala huo.
"Baada ya mafunzo haya yatafuata mafunzo ya siku tano kwa ajili ya walimu mahiri wa somo la lugha ya Kiingereza (English) katika halmashauri ya Chalinze kuanzia Novemba 21 hadi 25 yanayoshirikisha wawezeshaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, chuo cha Aghakhan, chuo cha ualimu Vikindu sanjari na mthibiti ubora wa Kanda."
Mafunzo hayo yatashirikisha viongozi wa elimu 42, walimu 100 kutoka katika shule teule za wilaya ya Chalinze na Kisarawe lengo likiwa ni kukuza uwezo wa walimu wa somo la Kiingereza wa Shule za Msingi kutekeleza mtaala mpya wa mwaka 2023
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.