Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepata mshauri mwelekezi kujenga bwawa kubwa kwenye Mto Rufiji eneo la Mloka ambalo litazalisha lita milioni 750 za maji kwa siku.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge alipokuwa akizungumza na wakazi wa Fukayosi mara baada ya kuzindua upanuzi wa mradi wa maji kwenye kata ya Fukayosi Wilayani Bagamoyo ambao kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo Mhandisi James Kionaumela umegharimu sh. milioni 350.3 mkandarasi akiwa ni Ms Shamoka Building and Civil Contructors Ltd. na utahudumia kaya 374 zenye watu 2,242 watakaopata huduma ya maji safi na Salama.
Alhaji Kunenge Alisema kuwa mradi huo wa Mloka Rufiji utasaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji kwa mkoa wa Pwani na Dar es Salaam pia kwa ajili ya wawekezaji, kilimo cha umwagiliaji na kwa wafugaji.
Katika hatua nyingine, Alhaji Kunenge ameagiza mkandarasi Civil Loth anayetekeleza mradi wa bwawa la maji katika Kitongoji cha Mjembe Kijiji cha Kwa Mduma Kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo kuripoti ofisini kwake kwa kushindwa kukamilisha mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 966 pamoja na kuwa aliomba na kuongezewa muda wa ziada wa miezi tisa.
Kunenge alisema mkandarasi huyo tayari alishalipwa kiasi cha shilingi milioni 483 sawa na asilimia 51.1 ya gharama za mradi lakini hajakamilisha kazi hiyo ambayo imefikia asilimia 73.
"Nilimpigia simu ili tukutane naye eneo la mradi lakini hajafika akidai yuko Mtwara namtaka aje ofisini Februari 16 ili atueleze changamoto yake ni nini inayomfanya ashindwe kukamilisha mradi kwa wakati licha ya kuongezewa muda," alisema Kunenge.
Akizungumzia mradi huo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani Mhandisi Beatrice Kasimbazi alisema kuwa changamoto kubwa ni mkandarasi huyo kutokuwa kwenye eneo la mradi huo wa Mjembe na Goe kwa muda mrefu na hata akiitwa kwenye vikao hafiki.
Kasimbazi aliongeza kuwa wanashindwa kuelewa mkandarasi huyo anakabiliwa na shida gani kwani wanapomwita kutaka kujua nini kinamkwamisha ili wamsaidie aweze kukamilisha mradi kwa muda aliopewa hatokei.
Diwani wa Kata ya Kibindu Ramadhan Mkufya alisema kuwa wananchi wa Kata hiyo kwenye Vijiji vyote wana shida kubwa ya maji hivyo mradi huo ungekuwa na manufaa makubwa kwao endapo ungekamilika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.