Ulega awasa wafugaji kuanzisha vyama vya Ushirika.
Waziri wa Mifugo na maendeleo ya Uvuvi Abdalla Ulega amewaasa wafugaji nchini kuanzisha na kujiunga na vyama vya Ushirika ili kupata tija katika uzalishaji, utunzaji na uuzaji mazao yatokanayo na mifugo ndani na nje ya nchi.
Aliyasema hayo alipotembelea na kukagua Machinjio ya "Union Meat Abattoir Ltd." yaliyopo kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo ameeleza kuwa Ushirika utawapa wafugaji manufaa ya kuinua na kuimarisha uchumi wa mfugaji mmoja mmoja na Taifa Kwa Ujumla.
Kufuatia ombi la Kampuni inayomiliki Machinjio hayo ya kupewa maeneo ya kukusanya na kulisha mifugo kabla ya kuingizwa machinjioni, Waziri Ulega ameiagiza kampuni ya Ranchi za Taifa Ltd (NARCO) kutenga eneo Kwa ajili hiyo na kuikabidhi kwa Kampuni hiyo mapema iwezekanavyo.
"Ninatambua maombi yenu ya kupatiwa eneo, ninaielekeza NARCO itoe eneo hilo haraka iwezekanavyo, apewe mwekezaji kabla ya msimu wa mvua ili aandae na kupanda malisho tayari kwa kupokea mifugo, mkataba na makabidhiano yakamilike mara moja ndani ya mwezi huu wa tisa kwani huu sio wakati wa danadana, ni wakati wa kuamua," amesema Ulega.
Pia waziri huyo kupitia machinjio hayo amewaasa vijana wanaopata ajira kwenye maeneo ya uwekezaji kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na bidii kubwa na kuepuka wizi huku akihimiza muwekezaji wa machinjio hayo kuweka viwango vizuri (gharama za huduma na bei za bidhaa) ili waweze kuwavutia wafanya biashara wengi zaidi wafikishe mifugo yao kuchinjwa hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa machinjio hayo Mariam Ng'wandu amesema wametumia Dola za kimarekani Milioni kumi (sawa na shilingi bilioni 26 za kitanzania) kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wake na wa Zahanati ya Kijiji cha Vigwaza na kwamba kitakamilika kwa ujenzi wa awamu tatu.
Naye mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon amesema kuwa Serikali imeweka miundombinu wezeshi na rafiki Kwa wawekezaji kama vile huduma za maji, umeme na Barabara ili kurahisisha uwekazaji.
Akiwa katika Kata ya Kwala Kijiji cha Mperamumbi kitongoji cha Msua Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Waziri Ulega amepata fursa ya kujionea uwekezaji wa uchimbaji wa bwawa la kunyweshea mifugo.
Hadi sasa ujenzi wa Bwawa hilo umegharimu kiasi cha shilingi milini 75.23, fedha hizo ni zilizochangwa na wafugaji ambao walitoa kiasi cha shilingi milioni 63.76, mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha shilingi milioni 10 na wadau mbalimbali shilingi milioni 1.51.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.