Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Nsajigwa Geoge ameeleza kuwa Serikali imefanya jambo kubwa na lenye tija kuanzisha mradi wa ukarabati wa reli ya kati wa awamu ya Pili kutoka Dar es Salaam hadi Isaka, mkoani Shinyanga (TIRP2).
Nsajigwa ameyasema hayo leo Julai 17, 2025 baada ya kupokea taarifa ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) iliyowasilishwa kwake na ujumbe wa shirika hilo uliyoongozwa na Mhandisi Dkt. Veronica Mirambo kwa lengo la kutambulisha mradi huo ambao unatarajiwa kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla.
“Mradi huu ni wa manufaa makubwa kwa wananchi. Mbali na kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo, pia utaongeza fursa za ajira kwa wananchi wa kada mbalimbali wakati wa utekelezaji wake,” alisema Nsajigwa.
Aidha Aliahidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi wa mkoa ili kuhakikisha kuwa shughuli zote za utekelezaji wa mradi zinafanyika kwa ufanisi.
Akiwasilisha taarifa ya shirika hilo, Mhandisi Dkt. Veronica Mirambo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Jamii kutoka TRC alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo una ushirikiano kati ya TRC na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufadhiliwa na Banki ya Dunia.
Alisema kwa sasa wako katika hatua za awali za kuanza utekelezaji wa Mradi huo ambapo timu ya wataalamu inatembelea maeneo yote yatakayohusika na ukarabati huo, ikiwa mkoa wa Pwani ni moja kati ya maeneo hayo.
Alisema lengo kuu la ukarabati wa reli hiyo ni kuboresha usalama, kuongeza ufanisi katika usafiri wa reli, pamoja na kuhakikisha miundombinu inakuwa imara na endelevu kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi katika kipindi chote cha uendeshaji.
Akibaninisha malengo mahususi kadhaa ya Mradi ni kuboresha njia ya reli na madaraja, kujenga mabwawa ya kupokea maji ya mvua ili kupunguza madhara ya mafuriko, na kuongeza uwezo wa kusafirisha abiria na mizigo ndani ya nchi na nje ya mipaka, hususan kuelekea nchi jirani.
Mradi huu pia utahusisha kuimarisha uwezo wa taasisi zinazohusika kama TRC, NIRC, LATRA pamoja na Wizara husika. Sambamba na hilo, mradi unalenga kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushiriki katika kutoa huduma za reli kupitia mfumo wa uwekezaji huria (open access).
Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuleta fursa mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo ajira kwa watu wenye ujuzi na wasiokuwa na ujuzi, kukuza biashara katika maeneo yanayopitiwa na reli, kurahisisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo, na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Vilevile, kupitia mabwawa yatakayojengwa, mradi huu utawawezesha wakulima kupata maji ya umwagiliaji, pamoja na wafugaji kupata maji kwa ajili ya mifugo yao, hatua ambayo inatarajiwa kusaidia kuboresha maisha ya jamii katika maeneo yanayopitiwa na mradi.
Shirika la Reli Tanzania linaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unazingatia viwango vya kimataifa na unawanufaisha Watanzania kwa kiwango cha juu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.