Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka viongozi wote wa Halmashauri za mkoa huo, kuainisha sekta zinazohitaji watumishi na idadi yake ili kuondokana na changamoto za ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inajengwa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo Juni 19, 2023 kwenye kikao kilichoketi na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG kwa halmashauri ya wilaya ya Kibiti kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Amewaelekeza Viongozi wa halmasahuri kuainisha vipaumbele vyao hasa katika eneo la watumishi kuwa waweke mahitaji yao kwa kuzingatia sekta zenye uhitaji ili maombi yapelekwe kwa mamlaka zenye dhamana ya kuwapanga watumishi wapya wapelekwe katika halmashauri hizo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia miradi kukamilishwa kwa wakati kuliko ilivyo sasa ambapo baadhi ya halmashauri inalipa fedha zote kwenye ujenzi wa miradi lakini inasuasua kwa sababu mikakati na vipaumbele vya mahitaji ya wananchi havijawekwa vizuri.
“Unakuta Fedha zinalipwa zote halafu miradi haikuendelea, inakuwaje tunalipa Fedha zote halafu miradi Haika kamili ka kisha unasema mradi unaendelea! Sasa Hili halivumiliki na halikubaliki, ili uweze kufanya malipo lazima uwe umejiridhisha ya kuwa mradi umekamilika kwa kiwango na ubora unaohitajika,” amesema Kunenge.
Ameongeza kufafanua kuwa “miradi inaanzishwa ili kutatua kero za wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu kama vile za afya, elimu, maji, usafiri na kilimo, hivyo usipokamilisha mradi unasababisha kero za ukosefu wa huduma hizo katika jamii na pia kuongeza gharama za utekelezaji na utakuwa umeihujumu Serikali na juhudi kubwa anazozifanya Mhe. Rais wetu kuwaletea wananchi maendeleo,” ameongeza Kunenge.
Amesisitiza kuwa jambo hilo halikubaliki na kwamba licha ya kuwa na changamoto ya wataalam katika baadhi ya sekta lakini suala la kutokamilisha miradi kwa wakati ni uzembe. “Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yetu inaumiza kuona wasaidizi wake wanakwamisha haiwezakani kila mmoja atimize wajibu wake,” amesema Kunenge.
Amesema halmashauri zikibainisha idadi ya watumishi kwa kuzingatia vipaumbele itasaidia kuajiri watumishi ambao watakwenda kutatua matatizo ya wananchi ambayo yanatokana na kutokamilika kwa wakati ujenzi wa miradi na uboreshwaji wa miundombinu mbalimbali ya kisekta.
Serikali inatoa fedha nyingi katika kukamilisha miradi ya maendeleo, fedha zote zinalipwa lakini changamoto ni miradi kutokamilika kwa wakati sasa jambo hili halifurahishi,”amesema Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.