Wazir wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa ametoa agizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hapa nchini kupita kwenye kila Halmashauri zote ambazo zimepata hati chafu kwa mujibu wa Mkaguzi na mdhibiti wa hesabuza Serikali na kufanya uchunguzi.
Mchengerwa alitoa agizo hilo April 26, Wilaya ya Rufiji alipokuwa kwenye ziara ya siku moja kuongea na watumishi wa Halmashauri ya Kibiti na Rufiji.
Alisema kuna haja ya Halmashauri hizo kufanyiwa uchunguzi ili kubaini watendaji wasiowaaminifu na hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema Halmashauri hizo zinatakiwa kufanyiwa uchunguzi ili ibainike sababu ya kupata hati chafu na waliohusika ili kuondoa watu ambao si waaminifu kwenye Utumishi.
"Takukuru kwenye maeneo ambayo Halmashauri zimepata hati chafu wafanye uchunguzi ili taarifa hizo zisaidie kuona sehemu ambazo hawakufanya vizuri na kama Kuna uzembe hatua zichukuliwe" alisema Mchengerwa
Mchengerwa pia aliwataka watendaji wa TAKUKURU kuhakikisha wanahudhuria kwenye mikutano inayoitishwa na wakuu wa Wilaya kwenye maeneo yao ili watoe elimu kwa wananchi.
Aidha Waziri huyo aliwataka viongozi wa Taasisi za Umma kushughulikia mashauri ya watumishi waliosimamishwa kazi waweze kupata haki zao kisheria.
Alisisitiza pia utolewaji wa mafunzo na semina kwa watumishi zitakazosaidia kuwajenga kuendelea kuwapa waadilifu kwenye Utumishi wao.
" Viongozi wa Taasisi, wakiwemo wakurugenzi tumieni ubunifu wenu kuwapatia mafunzo watumishi, zipo Taasisi ziko tayari kusaidia kutoa semina na mafunzo, wapeni fursa watumishi hii inasaidia kukumbushana masuala ya maadili kazini tisizibe fursa" alisema.
Mchengerwa alisema Serikali ya awamu ya sita imejipanga pia kuondoa kero za watumishi ambapo wanaostahili watapandishwa madaraja na kulipwa stahiki zao.
Alisema viongozi wa Taasisi za Umma wanatakiwa kufikisha taarifa za watumishi ambao hawajapata Shea madaraja ili ziweze kufanyiwa kazi kwa uharaka.
Waziri huyo pia alitoa onyo kwa watumishi wanaofanya kazi huku wakiwa na tabia ya ulevi na kuchelewa na kuwahi kutoka kazini kinyume na mkataba wa kazi kwani atakayegundulika hatua zitachukuliwa..
Awali mkuu wa Wilaya ya Rufijji Luteni Kanal Patrick Sawala alisema Wilaya hiyo ina upungufu wa watumishi zaidi ya 800.
Luten Kanal Patrick alisema kuwa katika Wilaya hiyo watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili walifukuzwa kazi ili kuimarisha Utawala Bora.
Mkuu huyo wa Wilaya alisemakati ya watumishi hao 10 ni kutoka idara ya Elimu Sekondari na watatu kutoka idara ya afya.
Alimuomba Waziri huyo kushughulikia kero zinazowakabili watumishi wa Wilaya hiyo ikiwemo ukosefu wa usafiri na vitendea kazi katika kutekeleza majukumu yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.