Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ametoa wito kwa wakulima wa maeneo ya mijini kutumia teknolojia ya kisasa katika kilimo na ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kipato chao.
Wito huo ameutoa leo Agosti 7,2025 wakati wa Maonesho ya Nanenane, katika Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Mnyema aliwahimiza wakulima wa mjini kutumia mbinu bora na za kisasa, ikiwemo matumizi ya nyavu kwa mazao yanayotambaa na ufugaji wa kisasa unaozingatia nafasi ndogo zilizopo mijini.
“Tunaamini kuwa kilimo cha mjini ni mkombozi mkubwa wa kipato kwa wananchi. Ni muhimu kutumia teknolojia na maarifa ya kisasa ili kuzalisha zaidi kwa tija hata katika maeneo madogo,” alisema Bi. Mnyema.
Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa jitihada zake katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia kwenye sekta ya kilimo na ufugaji, akibainisha kuwa juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa kilimo cha mjini.
Alisisitiza umuhimu wa wakulima na wafugaji kufuata ushauri na maelekezo ya wataalamu wa kilimo (maafisa ugani), ili kuimarisha uzalishaji na kusaidia kuhakikisha usalama wa chakula katika miji.
“Maendeleo ya kilimo mijini yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa wananchi na wataalamu. Tufuate ushauri ili tufanikiwe,” aliongeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.