Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo,amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa nchini ambao watawasilisha bajeti zao bila kutenga asilimia 10 kwa mujibu wa Sheria na kwamba bajeti zao hazitapitishwa.
Jafo alitoa angalizo hilo jana Mjini Kibaha alipokuwa katika kikao Cha kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Pwani ambacho kilijadili mpango wa bajeti ya mwaka 2020/2021 kwa Mkoa huo.
“Mkoa wowote, Mkuu wake wa Mkoa akileta taarifa ya mapendekezo ya mpango wa bajeti haitajadiliwa katika kikao cha kamati ya bajeti endapo haitaonyesha asilimia 10 iliyotengwa kwa mujibu wa Sheria" alisema.
Alisema kwenye taarifa ya bajeti kila mkuu wa mkoa atatakiwa kuwa na jedwali linaloonyesha namna Halmashauri zinavyotoa asilimia kumi kwa ajili ya mikopo ya makundi ya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu
Aidha alisema, hatakubaliana na Mkuu wa mkoa yeyote ambaye atakwamisha bajeti kwenye Wizara ya Tamisemi badala yake atapeleka majina kwa Rais kumueleza watu wanaokwamisha bajeti katika Ofisi yake.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato Jafo alisema, Mkoa wa Pwani bado hali hairidhishi kutokana na Halmashauri mbili pekee kati ya tisa ndizo zinazofanyika vizuri.
Kufuatia hali hiyo ametoa agizo kwa Wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia fedha zinazokusanywa kuingizwa katika mfumo wa Serikali.
Jafo alisema, mashine nyingi za kukusanyia fedha bado zinachezewa na kusababisha makusanyo yanayopatikana kutoingizwa katika mfumo wa Serikali.
Katika hatua nyingine Jafo alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya zote nchini kuainisha maeneo ambayo yameathiriwa na mvua zinazonyesha na kusababisha baadhi ya shule kufungwa.
Waziri Jafo alisema, ni vema maeneo hayo yakajulikana ili wanafunzi wanaosoma katika shule hizo watafutiwe mbadala waendelee na masomo hususani wale ambao wanamitihani ya kitaifa.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, alisisitiza kila Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vya ndani.
Kikao hicho kilipitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2020/2021 Shilingi Bilion 251.57.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.