Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewahimiza wananchi wa Mkoa wa Pwani kushiriki kikamilifu katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakaloanza Februari 13 hadi 19 mwaka huu. Wito huo umetolewa katika mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ukihusisha viongozi wa NEC na wadau mbalimbali wa siasa, dini, na jamii.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji (Rufaa) Mbarouk S. Mbarouk, alisema kuwa hadi Januari 16, 2025, uboreshaji wa daftari umekamilika katika mikoa 25, ikiwemo Kigoma, Tabora, na Katavi. Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi kwa wingi ili kuhakikisha kila mwenye sifa anaandikishwa na kuwa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi ujao.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Suleiman Mtibora, Mkoa wa Pwani unatarajiwa kuandikisha wapiga kura wapya 186,211, huku idadi jumla ya wapiga kura ikifikia milioni 1.18 baada ya zoezi hilo. Aliongeza kuwa vituo vya uandikishaji vitakuwa 1,913, ongezeko la vituo 179 ikilinganishwa na uandikishaji wa mwaka 2019/2020.
Wananchi pia wameonywa dhidi ya kujiandikisha zaidi ya mara moja, kwani ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni faini ya kati ya Shilingi 100,000 na 300,000, kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili, au vyote kwa pamoja.
Katika uboreshaji huu, NEC itatumia teknolojia ya kisasa ya Biometric Voter Registration (BVR) ili kuhakikisha usahihi wa taarifa za wapiga kura. Wadau wa uchaguzi wamehimizwa kushirikiana na NEC kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha kushiriki katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa demokrasia nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.