Wananchi Mkoani Pwani wametakiwa kutumia nishati mbadala badala ya mkaa ili kuweza kupunguza uharibu wa mazingira unaosababishwa na matumizi makubwa ya mkaa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo mwanzoni mwa wiki hii katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani .
Pia amewapongeza wananchi hao kwa juhudi za uhifadhi wa mazingira katika upandaji na utunzaji wa miti, ambapo jumla ya miti 7,716,819 imepandwa.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa utunzaji wa misitu unafaida kubwa ,kwani ni moja ya rasilimali inayoweza kuzuia mabadiliko ya tabia ya Nchi.
“Tukiharibu mazingira maana yake ni kwamba tunajiletea matatizo makubwa sana yakiwemo athari za mafuriko,kuongezeka kwa joto, kuongezeka kwa kina cha bahari pamoja na magonjwa mbalimbali na kukauka kwa vyanzo vya maji”alisema Ndikilo.
Aidha mhandisi Ndikilo alisema kuwa Suala la utunzaji wa mazingira linakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo uvunaji ovyo wa misitu,kilimo kisichozingatia kanuni bora za kilimo, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji na uchimbaji holela wa mchanga katika kingo za mito.
Katika Hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amepiga marufuku uchimbaji holela wa mchanga na ameagiza ifanyike tathimni ya mazingira ndipo leseni ya uchimbaji mchanga itolewe.
“Maelekezo ya Serikali ya Mkoa ili tuweze kupambana na uchimbaji holela wa mchanga katika Mkoa wetu wa Pwani hasa katika Wilaya za Mkuranga,Kibaha na Bagamoyo ni lazima sasa kabla kuchimba mchanga kwanza tathmini ya mazingira ifanyike vizuri ndipo leseni ya uchimbaji wa mchanga itolewe na mashimo yote yanayoendelea kuchimbwa sasa hivi maelekezo ya Serikali ya mkoa ni lazima Idara ya mazingira ngazi ya Halmashuri na ngazi ya Mkoa waendelee kuyafuatilia maeneo hayo ili kuona kuwa yako salama kwa ajili ya binadamu kwenye maeneo husika”alisema Ndikilo.
Maadhimisho ya kilele cha siku ya Mazinga Duniani kitaifa yalifanyika Mkoani Dar es Salaam na kwa Mkoa Pwani maadhimisho hayo yalifanyika Wilayani Mkuranga katika Kijiji cha Kisemvule yakiwa na kauli mbiu ya Mkaa ni gharama,tumia nishati Mbadala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.