Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge amewataka watumishi kufanya kazi zao kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi - CCM.
Hayo ameyasema leo Julai 10, 2023 wakati akizungumza kwenye kikao kati ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Katika mazungumzo yake, Kunenge amesema kuwa watumishi wa umma wana wajibu wa kutekeleza mipango ya maendeleo na kuondoa kero kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani hiyo.
Nae Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete katika kikao hicho amewaasa watumishi wa Umma kuacha tabia ya kusemana ovyo, kufitiniana na kufanyiana vituko na kuwa kufanya hivyo ni kuzorotesha utendaji kazi kwenye maeneo yao.
Aidha amewataka watumishi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuleta tija na kuacha alama.
"Naelekeza muachane na kasumba ya kusubiri kufuatiliwa na kusimamiwa kwenye majukumu yenu ya kazi, tekelezeni wajibu wenu bila kushurutishwa, fanyeni kazi kwa kujituma wenyewe," amesema Kikwete.
Nae Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta akitoa takwimu za watumishi ameeleza kuwa kwa sasa waliopo katika ofisi ya mkoa na za Wilaya ni 189 na upungufu ni 137.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.