Wakazi wa Changwahela ‘A’ Wilayani Bagamoyo wameitikia agizo la kutekeleza maelekezo ya Serikali la kuondoka katika eneo walilolivamia na kufanya shughuli za kibinadamu zenye uharibifu wa Mazingira.
Hali hiyo inafuatia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ambaye ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS, Mkoa wa Pwani kusimamia uhifadhi wa miti ya mikoko na kuzuia uharibifu wa mazingira uliofanywa na wananchi wa kitongoji cha Changwahela ‘A’ kilichopo Mapinga ambao wameamriwa kuondoka mara moja.
Kunenge alitoa agizo hilo wakati alipofika na kuzungumza na wananchi wa kitongoji cha Changwahela ‘A’leo Juni 7, 2023 katika kushughulikia changamoto zinazotokana na migogoro ya ardhi.
Akiwa katika eneo hilo, Kunenge amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanywa na wananchi hao ikiwamo ukataji hovyo wa mikoko ambayo inatunza kingo za bahari na kuhifadhi mazingira ya fukwe.
Amefafanua kuwa maagizo hayo ni utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na baraza la Mawaziri kufuatia ushauri wa timu ya mawaziri wanane wa kisekta iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2019/2020 ambao walishirikiana wataalamu kushughulikia migogoro ya ardhi mkoani humu na maeneo mengi nchini.
Kutokana na maamuzi hayo, Kunenge amemuagiza Kamishna wa Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kukaa na mwekezaji anayemiliki kiwanda cha Sea Salt na eneo lenye ukubwa wa ekari 600 ili waweze kumega ekari 50 n kuwapatia wananchi wa Changwahela ‘A’ ambao wametakiwa kuondoka eneo la mikoko.
“Nawaagiza TFS, kuanzia sasa simamieni eneo hili ambalo limeharibiwa na wananchi kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa kama vile uvuvi ambao umeharibu mikoko yetu na ujenzi wa nyumba 90 ambazo pia hazitakiwi kuwepo hapa hakikisheni uoto wa asili ulioharibiwa unarejea,” amesema Kunenge.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Changwahela, Kulwa Isdory amesema wamelipokea kwa mikono miwili agizo hilo na wapo tayari kuhama na kwenda eneo ambalo serikali imependekeza kuanza maisha mapya.
Akiwa Wilayani Bagamoyo, mkuu huyo wa mkoa pia alifika katika mtaa wa Sanzari Kata ya Magomeni na kuwaelekeza wakazi waliyovamia eneo la Yusuph Kikwete kupisha ili mwenyewe aweze kuendelea na shughuli za uwekezaji au wakae nae na kukubaliana watakavyoona inafaa.
Wakati huo huo, Kunenge ametoa muda wa siku 90 kwa Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo kukamilisha zoezi la urasimishaji makazi kwa ajili ya mpango wa matumizi ya ardhi kwa wananchi wa waliopewa eneo la ekari 5520 za Ranchi ya Taifa ya Ruvu.
Kunenge ametoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi wa kata ya Vigwaza kwenye mkutano wa hadhara, amedai kuwa zoezi hilo la urasimishaji makazi utavihusu vijiji 11.
Ameyataka maeneo ambayo yanahitaji urasimishaji kuwa ni Ruvu- Darajani- Bagamoyo ekari 500, Miro ekari 1000, Vigwaza ekari 20, Kidomole 100, Mkenge 100, Fukayosi 100, Kitonga 1200, Waja 1500 na Maguri 500.
“Baada ya kukamilisha taratibu zote kumega maeneo ya ranchi ya Ruvu nimetoa siku 90 kwa uongozi wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo kushughulikia ili wananchi wapate maeneo yao ambayo yametolewa na serikali, sitarajii kuona uvamizi wa maeneo mengine sasa,” amesema Kunenge.
Ziara ya leo ya Mkuu huyo wa Mkoa ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wake wa kushughulikia kero za wananchi zinazotokana na migogoro ya ardhi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.