Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI ,alhaj Selemani Jafo ,hajaridhishwa na ujenzi wa Ofisi ya halmashauri ya Chalinze ambao unasuasua tangu mwaka 2018 na kuagiza mkandarasi ambae ni Wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuondolea baada ya mei 31 mwaka huu.
Amemuelekeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo na wenzake wahakikishe awamu ya kwanza ya ujenzi inapokwisha mwezi huu watafute mjenzi mwingine wa majengo hayo .
Jafo alitoa kauli hiyo ,wakati alipokwenda kukagua na kujionea kasi ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya halmashauri ya Chalinze na halmashauri ya Wilaya ya Kibaha pamoja na hospital ya wilaya ya halmashauri ya Kibaha iliyopo Mlandizi.
Alisema ,kasi ya ujenzi huo ni mbaya ,haiendani na fedha ya bilioni 1.8 ya awamu ya kwanza ya ujenzi kwani ilipaswa wawe wamemaliza japo ghorofa moja .
"Ujenzi huu upo barabarani hapa ,halileti picha nzuri kabisa ,maana tangu mwaka 2018 ni nondo tu ndio zinachomoza ,majengo hayaishi ,haiwezekani kuendelea na TBA tena "alifafanua Jafo.
" Hatuwezi kuvumilia utaratibu huu wa zimamoto ,inaonekana kazi Leo inafanyika baada ya kujua ujio huu ,haiwezekani sasa miaka miwili ni hadithi tuu ,hatuwezi kwenda na mwenendo huu"
Aidha alikemea tabia ya wataalaamu wa ujenzi ,wahandisi kutokuwa na taarifa sahihi za ujenzi ambapo yeye anapokwenda kukagua na kuuliza maswali anamaanisha na sio kuanza kutafutiwa taarifa.
Nae mbunge wa Chalinze ,Ridhiwani Kikwete alieleza ,amekubaliana na maamuzi hayo kwani walishachoka kuona ujenzi haukamiliki kipindi kirefu sasa .
Ridhiwani alibainisha ifikie hatua tuache kufanya kazi kwa mazoea ,na tuheshimu fedha za umma kwa maslahi ya watanzania.
Meneja TBA mkoa wa Pwani ,Asha Muyanza alikiri kuchelewa kwa jengo ,lakini ni kutokana na ukosefu wa maji na gharama za vifaa ambavyo ilikuwa tofauti ambapo ujenzi ungekamilika mwaka 2018.
Kwa upande wake mhandisi wa halmashauri ya Chalinze, John Chizima alisema ujenzi ulipaswa ukamilike 2018 ,na gharama za ujenzi awamu ya kwanza ni bilioni 1.8 na hadi kukamilika kwa ghorofa tatu itagharimu kiasi cha sh .bilioni 5(tano ).
Baada ya kutembelea ujenzi huo alipata fursa ya kutembelea majengo ya ujenzi wa Ofisi ya halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ,Jafo ameridhishwa na ujenzi huo ambao utagharimu zaidi ya sh .bilioni nne .
Jafo alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Butamo na timu yake wasimamie miradi ikiwemo mradi wa hospital ya wilaya ukamilike kwa wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.