Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohammed Mchengerwa, ameipongeza Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha kwa kuendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa, hususan ya Kidato cha Sita na Kidato cha Nne.
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri Mchengerwa mwanzoni mwa wiki hii wakati wa ziara yake ya kikazi shuleni hapo, ambapo alikutana na uongozi wa shule hiyo na kujionea mazingira ya utoaji elimu pamoja na mafanikio yaliyopatikana.
“Nawapongeza sana kwa sababu Kibaha ni moja ya shule zetu maalum za Serikali ambayo haijashuka kiwango cha ufaulu. Wastani umeendelea kuwa wa juu, jambo linaloonesha juhudi za walimu na wanafunzi. Kwa hili, nawapongeza sana tena sana,” alisema Mhe. Mchengerwa.
Alisema katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka jana (2024), shule hiyo iliwawezesha wanafunzi wote 104 kufaulu kwa kupata daraja la kwanza (Division I), sawa na asilimia 100, huku wanafunzi 52 kati yao (asilimia 50) wakipata wastani wa juu zaidi wa Division 1.7.
Aidha, Mhe. Mchengerwa alionesha kuridhishwa na matokeo ya Kidato cha Sita ya mwaka huu (2025), ambapo wanafunzi 136 walifaulu kwa daraja la kwanza, sawa na asilimia 93.7 ya wanafunzi wote waliokalia mtihani huo.
Amesema si shule zote maalum zimekuwa zikifanya vizuri, na kuagiza Katibu Mkuu kufuatilia na kuchukua hatua kwenye shule zilizoshindwa kufikia viwango, akisisitiza kwamba Serikali haina nafasi kwa uzembe, hasa katika taasisi zinazobeba dhamana ya kutoa elimu ya viwango vya juu.
“Hatutaki kufanya mzaha kwenye eneo la elimu, hasa katika shule zetu maalum. Tupo tayari kuchukua hatua kali pale ambapo tunabaini uzembe au kushuka kwa viwango,” aliongeza Waziri Mchengerwa.
Ameeleza kuwa shule maalum kama Kibaha, licha ya kuwa chini ya TAMISEMI, zipo pia chini ya usimamizi wa mikoa, hivyo ni wajibu wa Mkuu wa Mkoa na timu yake kuhakikisha shule hizo zinasimamiwa ipasavyo ili ziendelee kuleta matokeo chanya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, Mwl. George Kazi, amesema walimu wa shule hiyo wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufanya vizuri zaidi. Alisema shule hiyo hufundisha masomo ya mchepuo minne: Sayansi, Biashara, na Kilimo.
Mwalimu huyo alifafanua kuwa mafanikio hayo yanatokana na nidhamu, ufuatiliaji wa karibu na maandalizi madhubuti ya wanafunzi tangu wanapojiunga na shule hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, alisema shule hiyo imeweka utaratibu wa kuwafanyia wanafunzi wa Kidato cha Tano mtihani wa majaribio mara baada ya kujiunga, ili kupima uwezo wao na kupanga mikakati ya kumudu mtaala ipasavyo. Aliongeza kuwa ufuatiliaji wa karibu kwa kila mwanafunzi umechangia kuifikisha shule hiyo katika viwango vya juu vya ufaulu kitaifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.