Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amewataka Maafisa Habari walioko chini ya TAMISEMI kuongeza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa taarifa kwa umma.
Mchengerwa alitoa wito huo leo, Mei 23, 2025, wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kinachowakutanisha Maafisa Habari kutoka Mikoa, Halmashauri, na Taasisi mbalimbali chini ya Ofisi ya Rais (ikiwemo DART, TARURA, TSC, Shirika la Elimu Kibaha na Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo), kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji, Mji wa Serikali, Mitumba – Dodoma.
Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa aliwakumbusha Maafisa Habari kuwa wanajukumu la msingi la kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za serikali kwa kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano.
“Serikali imefanya kazi kubwa kwa Watanzania, na kazi hizi zimefanyika katika maeneo yenu—katika mipaka ya Halmashauri, Wilaya na Mikoa yenu. Ninyi ndiyo mnaobeba ujumbe mzito wa sekta zote nchini,” alisema Mchengerwa.
Aidha, alibainisha kuwa msingi wa kuanzishwa kwa TAMISEMI ni kusogeza huduma na mamlaka karibu na wananchi, na kwamba utekelezaji mzuri wa dhamira hiyo unategemea Maafisa Habari kuwa kiungo muhimu cha utoaji taarifa katika maeneo yao.
Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za Serikali yametokana kwa kiasi kikubwa na juhudi za Maafisa Habari walioko katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambao wamekuwa wakitoa tafsiri sahihi ya shughuli zinazotekelezwa nchini.
Alifafanua kuwa Wizara yake inatekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia zaidi ya asilimia 21 ya bajeti ya nchi, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 11. Hivyo, utekelezaji huo unahitaji kuwasilishwa kwa wananchi kupitia mbinu za kisasa za mawasiliano na kwa kuzingatia teknolojia ya sasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.