Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka benki mbalimbali nchini ikiwemo benki ya maendeleo ya kilimo kutoa mikopo kwa vikundi vya kilimo ili viweze kupata fedha za kununulia matrekta.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuimarisha Sekta ya Kilimo ili kwenda sambamba na adhma yake ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Waziri Mkuu aliyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha kuunganisha matrekta cha URSUS-TAMCO kilichopo mjini Kibaha Mkoani Pwani.
Aidha amesema kuwa kiwanda hicho kinalenga kuboresha Sekta ya Kilimo nchini na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwanda kwa kuwa wakulima watakuwa na zana za kilimo za kisasa.
Pia amevitaka Vyuo vya Kilimo nchini kununua matrekta hayo kwa lengo la kufundisha wanafunzi wake ili wanapohitimu wawe na uwezo wa kutumia zana hizo vizuri na kwenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yao.
Waziri Mkuu ametia wito kwa Halmashauri nchini kuendelea kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya kilimo, uwekezaji, makazi, biashara na huduma za jamii ili kuepuka migogoro ya ardhi kwa siku zijazo.
Naye Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Bw. Mlingi Mkucha amesema wataunganisha matrekta 2,400, harrow 2,400, na majembe 2,400 katika mradi huo wa kiwanda cha kuunganisha matrecta cha URSUS-TAMCO ikiwa ni mkataba wa awali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili Sekta ya Viwanda Mkoani Pwani ni pamoja na kukatika kwa umeme mara kwa mara hivyo ameliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza vituo vya kupoozea umeme.
Awali Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage alisema kuwa, kwa sasa nchini kuna viwanda vikubwa 393, kati yake 84 viko Mkoani pwani ambapo amewaomba Viongozi wa Mkoa wa Pwani kutenga maeneo kwa ajili ya wanawake na vijana waweze kuanzisha viwanda vidogo.
Mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuunganisha matrekta cha URSUS-TAMCO ,Waziri Mkuu alitembelea pia eneo la uwekezaji la kamal(Kamal Industrial Estate ) lililoko katika kata ya Kerege Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.