Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salam Morogoro ambayo imefikia asilimia 77.91.
Majaliwa alibainisha hayo jana alipokuwa akiongea katika kituo cha soga Wilayani Kibaha wakati alipotembelea maendeleo ya mradi huo
Alisema kuwa kampuni ya Yap Merkezi imefanya kazi kama walivyosaini kwenye Mkataba na Serikali na naamini watakamilisha kazi kabla ya muda.
Waziri Mkuu huyo alisema, reli hiyo itatembezwa na umeme kutoka katika chanzo cha Kidatu Morogoro, Bwawa la Mwalimu Nyerere Rufiji pamoja na Kinyerezi ambacho kitakuwa kinatumia gesi.
" Reli haitasimama kwa kukosa umeme, mbali ya vyanzo hivi vitatu pia mabehewa yatakuwa na uwezo wa kutunza umeme kwa dakika 45 ikitokea ukakatika kwenye vyanzo vyote Jambo ambalo hatutarajii litokee" alisema Majaliwa.
Akizungumzia ajira kwenye ujenzi huo alisema, katika eneo la Dar es Salam Morogoro ajira 7400 zilitolewa na Morogoro Makutupora watu 6300 walinufaika na ajira.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema, ni matarajio ya Serikali ifikapo mwezi Mei 2021 reli hiyo ianze kufanya kazi, ambapo inadaiwa treni ya abiria itakiwa na uwezo wa kubeba abiria 560 hadi 600.
Katika hatua nyingine Majaliwa amewataka wananchi kuchukua taadhaali na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kujikinga na virusi vya Corona kwani hakuna dawa ambayo imepatikana hadi sasa.
Nae Naibu Waziri Ujenzi na Mawasiliano Atashasta Nditie alisema kuwa lengo la ziara hiyo ya Waziri Mkuu ni kuangalia maendeleo ya mradi huo na utayari wake wa kuanza kazi katika kipindi Cha miezi miwili ijayo.
Nditie alisema, kuna vitu vidogo vilibakia ambavyo vilisimama kutokana na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Alisema reli hiyo ya kisasa itakapokamilika wananchi watafanya safari kwa haraka na ambapo kutoka Dar es Salam hadi Morogoro itakuwa kwa muda ea saa 1.30.
Aidha Naibu Waziri huyo alisema, treni hiyo ya kisasa ina faida za kiusalama kwani kila itakapokuwa inajulikana maeneo yote inayopitia.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli Masanja Kadogosa alisema kuwa ,gharama ya ujenzi wa mradi huo wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salam hadi Makutopora Singida utagharimu kiasi cha Shilingi trilion 7 hadi kukamilika.
Kadogosa alisema, hadi sasa ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salam hadi Morogoro kwa urefu wa kilomita 300 umekamilika kwa asilimia 77.9.
Mkurugenzi huyo alisema, mvua zinazoendelea kunyesha hapa chini zilikwamisha baadhi ya kazi kukamilika kwa wakati.
Meneja Mradi msaidizi Mhandisi Ayoub Mdachi alisema,treni ya mizigo itakuwa na uwezo was kubeba tani 10,000 kwa mara moja, na itakuwa na uwezo was kutembea kilometa 120 kwa saa wakati treni ya abiria ikitembea kilomita 160 kwa saa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.