Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, leo amezindua Bodi mpya ya Afya na Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi, na kuagiza bodi hiyo kusimamia vyema utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Pia, aliihimiza kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto kwa kuzigeuza kuwa fursa zitakazosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya. Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Aidha, Mhe. Mhagama alisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi, pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali watu ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma.
Tunataka tunapofanya tathmini tuone mabadiliko chanya kwa kutumia changamoto zilizopo kama fursa ya kubuni njia mbalimbali zitakazoboresha huduma za afya katika hospitali zetu. Natarajia Mwenyekiti afanye kazi nzuri ili tuje kujifunza kutoka kwake,†alisema Mhe. Mhagama.
Aliwataka pia wajumbe wa Bodi hiyo, inayoongozwa na Bi. Zalia Mbeo kama Mwenyekiti, kufanya kazi kwa uzalendo, weledi, na ufanisi ili kuongeza tija katika sekta ya afya.
Vilevile, Mhe. Mhagama alitembelea viwanda vya dawa vya Action Medeor, Katwaza Pharmaceutical Industry, na Kairuki Pharmaceutical Industry, ambapo alikiri juhudi kubwa zilizofanyika katika sekta hiyo. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza tafiti za kisayansi ili kuzalisha dawa zaidi nchini, hatua itakayopunguza utegemezi wa dawa kutoka nje na kupunguza gharama kwa serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, alipongeza jitihada za uwekezaji katika sekta ya afya zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alibainisha kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2021 hadi sasa, Mkoa wa Pwani umepokea zaidi ya shilingi bilioni 37 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya na bilioni 5 kwa ununuzi wa vifaa tiba.
Jitihada hizi zimewezesha ongezeko la vituo vya afya 156, na hivyo kufanya Mkoa wa Pwani kuwa na zaidi ya vituo 500 vya kutolea huduma za afya, hatua inayoboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.