Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, amepokea wageni kutoka Jimbo la Jilin nchini China, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Bwana Gao Guangbin. Ujumbe huo upo nchini kwa madhumuni ya kushirikiana na Mkoa wa Pwani katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi na kubadilishana uzoefu.
Mheshimiwa Kunenge ameeleza kuwa ziara hii imefuatia ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini China iliyofanyika tarehe 4 Septemba mwaka huu, ambayo ililenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili na kuongeza fursa za uwekezaji nchini.
“Safari za Mheshimiwa Rais zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu, kwani zinaleta fursa za uwekezaji kutoka kwa wafanyabiashara na makampuni makubwa, jambo ambalo linaongeza tija kwa wananchi wetu,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa wageni hao wamevutiwa na fursa za kiuchumi zilizopo Mkoa wa Pwani, kufuatia utafiti waliofanya. Pia, alisisitiza kwamba Pwani ina rasilimali nyingi zinazovutia uwekezaji katika sekta kama kilimo, utalii, viwanda, uvuvi, ufugaji, na uchumi wa bahari.
Aidha, Mheshimiwa Kunenge alieleza kuwa Mkoa wa Pwani utapata fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu na kujifunza mbinu bora za kuendesha shughuli za kiuchumi. Alifafanua kuwa, baada ya ziara hii, wataandaa timu maalum ya kupanga maeneo muhimu ya uwekezaji na kuandaa mikakati bora ya utekelezaji wa mpango kazi wa uwekezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.