Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dkt Delphine Magere ameipongeza timu ya wataalamu wakitanzania wanaosimamia ujenzi wa mradi wa bwawa litakalotumika kuzalisha umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) kwa jinsi wanavyojituma kutekeleza majukumu yao.
Dkt.Magere alitoa pongezi hizo alipofanya ziara kujionea hali ya maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo ambalo hadi sasa ujenzi wake unaendelea kwa kasi.
”Tumekuta mradi ukiendelea vizuri kutokana na usimamizi mzuri wa wataalamu weenyeji, tumeiona faida ya kazi kusimamiwa na weenyeji, huu ni mmoja kati ya miradi michache inayosimamiwa na watanzania na inaendelea vizuri, ninawapongeza sana” alisema Dkt. Magere.
Katika ziara hiyo, Dkt. Magere alishuhudia na kupata maelezo ya kazi za ujenzi wa handaki la kuchepusha maji (diversion tunnel), tuta kuu (main dam), kingo ndogo za kuzuia maji (saddle dams), jengo la mitambo (power house), mitambo ya kuzalisha umeme (electromechanical Equipment), kituo cha kupokea na kusafirisha umeme (400kV switchyard) na daraja la kudumu (permanent bridge),
Kazi zingine katika mradi huo ni za ujenzi wa barabara za kudumu (Permanent roads), nyumba za makazi 113 (employee’s operation village), uchimbaji na uimarishaji wa kingo pamoja na ujenzi wa njia ya kupeleka maji katika mtambo (water way).
Dkt. Magere alitoa wito kwa halmashauri za Wilaya zinazopitiwa na mradi huo kuwa na ubunifu wa kuandaa mazingira mazuri yatakayosaidia kutunza vifaa vya utekelezaji wa mradi huo na kujiongezea mapato ya ndani kutokana na shughuli mbalimbali zinazohitaji gharama.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Mushubila Kamuhabwa alieleza kuwa tayari watanzania wameanza kufaidika nao katika hatua za awali kwa kupata ajira ambapo tayari wameajiriwa wafanyakazi 4,027 kati ya wafanyakazi 6,000 wanaohitajika na wengi wao wakiwa ni weenyeji wa vijiji vya maeneo ya jirani kama Mloka na Kisaki.
Mhandisi Mushubila aliongeza kuwa mradi huo pia umechochea matumizi ya bidhaa na huduma mbalimbali za hapa nchini kuweza kununuliwa na kutumiwa kwenye ujenzi huo.
“Makampuni na viwanda vya ndani vinauza bidhaa zao hapa na mfano ni saruji tani 850,000, nondo tani 70,000 pazolana tani 250,000 inanunuliwa kutoka kwa watoa huduma wa hapa hapa nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wetu” alisema Mhandisi Mushubila.
Akifafanua manufaa ya mradi huo utakapokamilika, Mhamdisi Mushubila alisema kuwa utadhibiti mafuriko kwenye maeneo ya ukanda wa chini ya bwawa, utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, utasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu kwa wataalamu wa ndani katika kujenga na kusimamia miradi kama hiyo, kutakuwa na ongezeko la mapato ya TANESCO kwa uuzaji wa umeme utakaozalishwa kwa gharama nafuu, ongezeko la mapato ya serikali yatakayotokana na tozo mablimbali, ongezeko la upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na wanyama na uvuvi endelevu katika bwawa la mradi.
Alifafanua manufaa mengine kuwa ni kuanzisha aina mpya ya utalii wa majini, manufaa katika ekolojia, kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika eneo lenye ukubwa wa takriban hekta 1,500,000, kuzipatia soko bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani na kuongeza ajira.
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.