Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Theresia Mmbando ameziagiza Halmashauri za mkoa huo kusimamia kikamilifu makusanyo ya Mapato ya ndani, Mifumo ya Fedha, Matumizi ya Fedha na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yao ili kufanikisha malengo ya Halmashauri.
Mmbando alitoa maagizo hayo mwanzoni mwa wiki wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili mrejesho wa ziara za ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Halmashauri za Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na Watendaji toka ofisi ya mkuu wa Mkoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waweka Hazina na wataalamu wa Mifumo ya Mawasiliano na Teknolojia.
Akifafanua umuhimu wa usimamizi wa makusanyo ya mapato ya ndani, Aidha alieleza kuwa ndio chanzo cha fedha za uhakika ambazo kila Halmashauri inaweza kujivunia kutekeleza shughuli zake za kila siku.
“Takwimu za makusanyo za mwaka wa fedha 2018/19 zinaonesha Halmashauri tatu tu ndizo zimekusanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze (asilimi 133), Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga (asilimia 129) na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imefikisha (asilimia 114), Nawapongeza sana, Halmashauri ya Mji Kibaha imefikia asilimia 94 tunaipongeza pia hongereni na ongezeni bidii kufikia lengo” alisema Mmbando.
Katibu tawala huyo alibainisha kuwa Halmashauri tano hazikufikia asilimia 80 ya makusanyo ambacho ndio kigezo kilichowekwa cha kuzifanya ziendelee kuwepo na akazitaja na asilimia zao kwenye mabano kuwa ni Bagamoyo (65), Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (57), Kibiti (66), Mafia (62) na Rufiji (75).
Kutokana na hali hiyo, Bi. Mmbando ameagiza kuwa kila Halmashauri ihakikishe kuwa inakuwa na kanzi data (database) ya uhakika wa walipa kodi/ushuru, Kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, Kuongeza udhibiti wa Vyanzo vinavyofanya vizuri sasa hata ikiwezekana kuweka “CCTV” kamera katika vituo vya ukaguzi, Kuongeza mashine za kukusanyia mapato na kusimamia matumizi yake, Kubuni miradi ya Kimkakati itakayoongeza mapato na Kutumia mapato ya sasa kuwekeza katika Miradi ambayo itaongeza mapato katika Halmashauri.
Akizungumzia Usimamizi wa Mifumo ya fedha, Bi. Mbando alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa miaka mitatu, imejitahidi kuweka Mifumo ya fedha ambayo ni wa Mapato (LGRCIS), Mfumo wa taarifa za Hospitali (GoTHoMIS) na Mfumo wa Taarifa za Fedha za Vituo vya Kutolea huduma (FARRS) katika Halmashauri kwa lengo la kusaidia kusimamia na kudhibiti Mapato na Matumizi,.
Ili kufanikisha malengo ya mifumo hiyo, Bi Mmbando ameziagiza Halmashauri kuhakikisha kuwa Vituo vya Afya na Zahanati vinafungwa mfumo wa GoTHoMIS hadi Desemba 2019, Kukamilisha uunganishaji wa Mfumo wa Hospitali maeneo yote ya huduma, Kusimamia matumizi ya mifumo yote vizuri na Wakurugenzi kufuatilia matumizi ya Mfumo wa GoTHoMIS na kuona kama unasaidia kudhibiti mapato na Taarifa zitolewe.
Kwa upande wa Usimamizi wa matumizi ya Fedha, Bi. Mmbando alizipongeza Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kwa kupata Hati safi kwa miaka mitatu mfululizo na akazitaka kuendeleza juhudi hizo bila kurudi nyuma.
Pia aliziasa Halmashauri kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kufuata mpango na bajeti ambao umepangwa kwa mwaka zikizingatia Sheria za fedha na taratibu za ununuzi pamoja na kanuni zake.
Katika kuziwezesha Halmashauri za mkoa wa Pwani kuendelea kufanya vizuri kwa usimamizi wa matumizi ya fedha Bi Mmbando ameziagiza kutoa maelezo na vielelezo kwa Hoja zilizobaki kama zilivyowasilishwa na CAG ili ziweze kufungwa kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba 2019 na zisionekane kwenye ukaguzi ujao.
Maagizo mengine katika eneo hili ni Kuepuka kuzalisha Hoja, Kuanzisha na kuimarisha kitengo cha ukaguzi wa awali kabla ya malipo, Timu yote ya Menejimenti ishiriki Vikao vya CAG wakati wa Ukaguzi, Mkurugenzi kutoa umuhimu zoezi la ukaguzi na kushiriki kwenye vikao vya “Entry” na “Exit” yeye mwenyewe, Menejimenti iwe inajiwekea muda maalum wa kujibu na kutolea ufafanuzi kasoro zinazobainishwa na CAG baada ya Kikao cha kumaliza ukaguzi, Mkurugenzi Kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote waliosababisha hasara kwa Halmashauri mapema ili kulinda nidhamu ya kazi, kuongeza uwajibikaji na Kuimarisha kitengo cha ukaguzi wa ndani na kufanyia kazi kasoro zinazobainishwa kwa wakati.
Bi. Mmbando pia alizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa akizitaka Halmashauri kufanya maandalizi ili kufanikisha shughuli zote za kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na akaagiza kuwa Shughuli zote zinazotakiwa kufanyika ziainishwe kabla ya uchaguzi na kuzipangia ratiba ya utekelezaji na kuonesha muhusika wa utekelezaji, Kuundwa kamati maalum ya maandalizi ya uchaguzi katika ngazi ya Halmashauri na kwamba Mkoa utafuatilia maandalizi katika kila Halmashauri ili ziendelee kufanya vizuri katika uchaguzi.
Katika kikao hicho, mada zilizowasilishwa ni pamoja na Tathmini ya uandaaji wa Mpango Mkakati na maandalizi ya taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo (CDR), Muhtaasari wa taarifa za ukaguzi, changamoto za matumizi mifumo ya fedha, changamoto za makusanyo ya mapato ya ndani na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.