Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Uvuvi, na Mifugo imefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Pwani kwa kutembelea Maabara ya Uzalishaji wa Chanjo ya Mifugo ya TVLA iliyopo wilayani Kibaha.
Kamati hiyo ilipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, ambaye, pamoja na mambo mengine, alizungumzia mikakati mikubwa iliyowekwa na Serikali ya Mkoa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na kuvutia uwekezaji ndani ya mkoa.
Mheshimiwa Kunenge alieleza kuwa mikakati hiyo inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, Bandari Kavu ya Kwala, ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo, na kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika pamoja na gesi.
Katika ziara hiyo, Kunenge aliomba Serikali kuongeza juhudi katika ujenzi wa miundombinu katika kongani za viwanda ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, hatua itakayosaidia kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika maeneo hayo.
Aidha Kamati hiyo iliyoongozwa Mwenyekiti wake, Mhe. Deodatus Mwanyika imeipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa uzalishaji wa chanjo za mifugo ambazo zinatumika kukinga magonjwa mbalimbali pamoja na kuboresha afya za mifugo hapa nchini.
Pongezi hizo walizitoa wakati walipotembelea Wakala ya Maabara hiyo ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwenye Taasisi ya Chanjo Tanzania
‘Leo tumetembelea Maabara hii ya uzalishaji wa Chanjo, tumeangalia kazi zinazofanyika hapa, tumelizika kwa kiasi kikubwa, tunaipongeza sana Serikali, na tunaipongeza sana TVLA. Kamati tunataka watu waelimishwe kuhusu umuhimu, uzuri na uhitaji wa chanjo ili wasiwe na wasiwasi kuhusiana na chanjo zetu. Chanjo ni muhimu kwa mustakabali mzima wa ufugaji’ Alisema Mhe. Mwanyika
Kwa upande wake Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema kuwa mipango ya Wizara ni kuendelea kuhamasisha pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kuchanja Mifugo kwani kuna baadhi ya wafugaji hawana utaratibu wa kuchanja.
‘Tuna maafisa ugani kwenye ngazi ya kata na kijiji na halmashauri wote wanaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo na uchanjaji, chanjo zipo za kutosha, tuwahakikishie wafugaji wote kuwa tuna uwezo wa kuzifikisha popote walipo’ Alisema Mhe. Mnyeti
Pia, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya VeterinariT anzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi amesema kuwa kwa sasa TVLA imeweza kuwafikia wafugaji moja kwa moja kuwapa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa mifugo yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.