Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeupongeza mkoa wa Pwani kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa mkoani humo kukuza uchumi wa Taifa.
Akitoa pongezi hizo kwenye kikao kifupi kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani leo Machi 14, 2024, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Rashid Kawawa amesema kuwa mkoa wa Pwani unaenda kuwa kitovu kikubwa cha uchumi kutokana na ongezeko la viwanda na uwekezaji kwa sekta mbalimbali katika kila eneo la mkoa huo.
Amesema hali hiyo inatokana na jitihada zinazofanywa na viongozi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa kuna utulivu na amani hivyo kuwavutia wawekezaji ambao hitaji lao kubwa ni usalama.
"Sisi tunaridhika sana kwa sababu hatujapata malalamiko yoyote, labda yale ya kimazingira na yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi," amesema.
Ameeleza kuwa iwapo hali ya usalama itaendelea ilivyo, wawekezaji wengi watafika kuwekeza na kulipatia taifa manufaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali kupata kodi huku vijana wakipata ajira.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa taarifa kuwa hali ya kukua kwa kasi ya ongezeko la viwanda na uwekezaji unatokana na sera nzuri za nchi na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwatafuta wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma mbalimbali kama Umeme, maji na miundombinu ya barabara, Kunenge ameeleza kuwa mkoa alishatoa maelekezo kuwa mipango ya taasisi zote za serikali lazima iendane na mipango ya Mkoa na kwamba huduma yoyote inapopelekwa mahala, basi ihudumie wateja wengi zaidi.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imeushauri uongozi wa Moa wa Pwani kufikiria kuboresha barabara za pembezoni (za mchepuko) ya barabara kuu ya Dar es Salaam - Chalinze ili ziweze kupunguza tatizo la msongamano na ajali kwa wakati huu ambao maandalizi ya ujenzi wa Barabara ya Kulipia ya njia nne kutoka Kibaha - Morogoro "Express Way" yakiendelea.
"Tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa vile linafanya kazi kubwa kwenye barabara hiyo kuhakikisha usalama wa watjmiaji unakuwepo," amesema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.