Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa amani na utulivu ili kuhakikisha wanapata viongozi bora.
Dkt. Mpango alitoa rai hiyo wakati wa sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2025, zilizofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
“Kama kauli mbiu yetu inavyosema, mwaka huu, 'Shiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.' Tujitokeze kwa wingi katika kutumia haki yetu ya msingi na kuchagua viongozi wetu kwa amani na utulivu,” alisema Dkt. Mpango.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa uhuru na haki, ili kuwawezesha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
Aidha, aliwasisitiza wakimbiza Mwenge wa Uhuru kukagua miradi kwa ustadi na kutokusita kufichua ubadhilifu wa mali, fedha, pamoja na wala rushwa bila woga.
Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais kuzindua Mwenge wa Uhuru, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema aliridhishwa na maandalizi ya sherehe hizo na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Abubakar Kunenge pamoja na Kamati ya Maandalizi. Waziri Mkuu aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika mikoa 31 na kukagua miradi 195.
Pia alisisitiza Amani na Utulivu, kama kaulimbiu inavyosema, ni muhimu katika kuendeleza juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa nchi. "Amani na utulivu ndio msingi wa maendeleo yetu, bila Amani na utulivu hakuna maendeleo," alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema kuwa katika kipindi chote cha mbio hizo, Mwenge wa Uhuru utahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Jitokeze Kushiriki Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema utakimbiza katika Halmashauri zote tisa na Wilaya saba za Mkoa wa Pwani mwenge na utapitia na kukagua miradi 64 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.028.
Mara baada ya kuzinduliwa, Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake katika Mkoa wa Pwani, ukikimbizwa katika Manispaa ya Kibaha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.