Wakazi wa Wilaya ya Rufiji, Mkoani Pwani pamoja na watanzania kwa ujumla wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Hydropower Dam Project), ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 2,100. Mradi huo utazalishwa kutoka chanzo hicho , katika pori la akiba la Selous kanda ya kaskazini (Matambwe). Kwasasa nchi inazalisha megawatts 1,450 lakini Stiegler’s gorge itazalisha megawatts 2,100 hali itakayoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi .
Akizungumza mara baada ya kwenda kukagua na kujiridhisha eneo utakapozalishwa mradi huo kabla ya utekelezaji kuanza, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist W. Ndikilo, alisema tangazo rasmi limeshatolewa na Wizara ya Nishati na Madini tangu mwezi tarehe 30/08/2017. Aidha alifafanua kuwa, tangazo hilo linawapa nafasi kwa makampuni ya ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.
Mhandisi Ndikilo, alibainisha kampuni yoyote iwe ya ndani ama nje ya nchi ikikidhi vigezo itatangazwa. Alieleza endapo mradi utakamilika utawezesha kuwepo kwa umeme wa uhakika na kuvutia wawekezaji kwa wingi. Wilaya ya Kisarawe na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Kibiti na Rufiji kuna changamoto ya upungufu wa umeme hali inayokwamisha jitihada za kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda .
“Tatizo la umeme bado ni kubwa Mkoani hapa licha ya Mkoa huu kusheheni viwanda “Mradi umekuja muda muafaka ambapo Mkoa huo umejipanga kuwa ukanda wa viwanda ” alifafanua.
Aidha Mh.Ndikillo alisema kwamba mradi umekuja muda muafaka na umefika mahala pake , ambapo Mkoa huo umejipanga kuwa ukanda wa viwanda .
“Ni nia ya Serikali ya awamu ya tano kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka katika maporomoko ya mto huo yanatekelezwa kwa haraka iwezekanavyo “ alisema mhandisi Ndikilo .
Baada ya kutembelea eneo la mradi Mhe. Ndikilo, alipata fursa ya kwenda kuzungumza na wakazi wa Kijiji cha Mloka kilicho mpakani mwa pori la akiba la Selous. Hata hivyo Mhe. Ndikilo, alisema kuwa ujenzi wa mradi huo utafungua milango ya kiuchumi, ujasiriamali na kibiashara.
Eneo litakalotumika kujenga mradi ni kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia tatu pekee ya eneo lote la pori la akiba la Selous yenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000.
Mkuu wa pori hilo kanda ya kaskazini (Matambwe) Bw. Lawrence Okode, alisema katika historia jina la Stiegler’s Gorge limetokana na Mjerumani aliyefariki katika eneo hilo aliyejulikana kwa jina la Stiegler’s baada ya boti yake kugonga jiwe kubwa na kusababisha umauti wake .
Kwa upande wa wakazi wa Mloka, Ikwiriri na Kibiti waliridhia na kuonyesha kukubali maendeleo wanayosogezewa. Mkazi wa Mloka Mzee Mbonde, alisema alikuwepo enzi za Hayati Baba wa Taifa wakati mradi ulipofanyiwa tathmini na watu wa Norway. Mzee Mbonde na Bibi Fatuma Majengo walimpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Walisema kwa mwanzo huu, Mhe. Magufuli atatatua tatizo la uhaba wa umeme.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.