Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amesema maandalizi ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 yamekamilika, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikihimiza Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 26, 2025, Ridhiwani alieleza kuwa vijana sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wameandaliwa kwa ajili ya kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika jumla ya Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195.
“Kwa kipindi chote hicho, Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuwahimiza wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Ridhiwani.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.” Waziri alisisitiza kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru imekuwa kiini cha historia muhimu ya taifa, ikiwemo Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huo huo, na Azimio la Arusha la 1967.
Uzinduzi wa mbio hizo utafanyika Aprili 2, 2025, katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, amesema maandalizi yako katika hatua za mwisho na yatakamilika ifikapo Machi 29, 2025.
Mwenge wa Uhuru, ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961, unaendelea kuwa alama ya mshikamano na maendeleo ya taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.