Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Baran Sillo, Januari 10, 2025, alitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Abubakar Kunenge. Mazungumzo yao yalijikita katika masuala ya usalama na uboreshaji wa huduma za msingi kwa Jeshi la Polisi na wananchi.
RC Kunenge aliwasilisha ombi la mkoa wake kuongezewa askari wa barabarani, gari la zimamoto, na vifaa vya kazi kwa askari wa barabarani. “Tunaomba msaada wa kuongezewa gari la zimamoto ili kusaidia hali ya dharura, hasa kwa kuwa Pwani ni mji wa viwanda. Pia, tunahitaji kuongeza askari wa barabarani na vifaa vyao, kwa sababu barabara yetu ya Morogoro ni nyembamba, na mara nyingi ajali zinazotokea zinahitaji usaidizi mkubwa,” alisema Mhe. Kunenge.
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka kipaumbele kwenye upanuzi wa Barabara ya Morogoro, akibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo utaanza hivi karibuni.
Kunenge pia alimhakikishia Naibu Waziri kuwa hali ya usalama mkoani Pwani ni ya kuridhisha, huku akipongeza Jeshi la Ulinzi na Usalama kwa juhudi zao za kulinda raia na mali zao.
Baada ya kikao hicho, Mhe. Sillo alitembelea Kituo cha NIDA Kibaha (Data Center), ambako alitarajiwa kuzungumza na watumishi wa kituo hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.