Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezielekeza halmashauri za mkoa huo kumaliza migogoro ya ardhi ili kuwezesha kuongeza kasi ya uchumi kukua na kupanuka hali itakayoziwezesha kuongeza mapato yao.
Kunenge ameyasema hayo kwa nyakati tofauti kwenye vikao vya mabaraza ya Halmashauri ya Kibaha Mji na Bagamoyo kujadili hoja za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali vilivyofanyika kwenye kumbi za halmashauri hizo Juni 24, 2024.
Amezieleza halmashauri hizo kuwa Bila kumaliza migogoro ya ardhi hawawezi kuwa na maeneo ya kufanyia shughuli za kiuchumi na hivyo kuzorotesha maendeleo ya wananchi.
"Mapato yanatengenezwa, yanakusanywa na kupangiwa matumizi kwenye maeneo yenye vipaumbele, mapato ni akili, tengeneza mapato mwenyewe hivyo bila kumaliza migogoro ya ardhi hauna maeneo ya kufanyia shughuli za uchumi," amesema.
Kuhusu hali ya halmashauri hizo kufanikiwa kufikia au kuvuka lengo la asilimia za ukusanyaji wa mapato, Kunenge amewaasa kutoridhika na hali hiyo kwa kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya huduma kwa wananchi kwani kila mwaka malengo yanaongezeka kutokana na idadi ya watu kuongezeka.
"Watoto wanazidi kuzaliwa, kuna mahitaji kama madarasa, vituo vya kutolea huduma za afya, mahitaji ya maji, miundombinu, haya yote yanahitaji mapato hivyo wekeni jitihada na mikakati ya kuongeza ukusanyaji.
Alihoji kwanini halmashauri zinakuwa na tofauti ya makusanyo na halamashauri zingine kwa kufuata mipaka ya kiutawala huku zikiwa na fursa lukuki akisema, "hakuna laana ya makusanyo ya mapato yanayozingatia mipaka, mnapakana na halmashauri zenye mapato makubwa, kwanini nyie mkusanye kidogo?" amehoji Kunenge.
Katika mikutano hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta mbali na kuzipongeza halmshauri hizo kwa kupata hati safi na kwa kuvuka lengo la makusanyo, amezielekeza kumaliza hoja zilizobaki.
Mchatta pia amezelekeza halmashauri hizo kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kutumia vitendea kazi kama vile vishikwambi na matumizi ya mifumo kama ule wa e-office na mingine ili kuondokana na matumizi ya karatasi.
Naye Mkaguzi wa nje Mkoa wa Pwani toka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi CPA Pastory Masawe amezipongeza halmashauri hizo kupata hati safi na akazitahadharisha kutobweteka na kuharibu hiyo sifa ambayo kwa halamashauri ya Kibaha Mji imeendelea kuwepo tangu ianzishwe.
Na amewaasa kuendelea kufanya maboresho kwenye makusanyo na matumizi.
"Kuna maeneo ambayo ni pamoja na ukusnyaji na kusimamia mapato, kukusanya ni jambo moja lakini kutumia pia ni jambo lingine, kile tunachokikusanya tujaribu kukitumia vizuri," amesema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.