Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza watumishi wa Umma na sekta binafsi mkoani humo kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.
Ndikilo alitoa agizo hilo mjini Kisarawe akiwa katika mkutano na wakazi wa mji huo, katika ziara yake ya kikazi kusikiliza kero za wananchi anahoifanya Mkoani humo akiambatana na kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, pamoja na wayendaji.
"Tusisubiri viongozi wa ngazi ya kitaifa wafike kutatua kero za wananchi kwenye vitongoji na kata hii si sawa, jipangeni kuwasikiliza wananchi na kutafuta ufumbuzi wa vikwazo vya maendeleo kwao na pia mnapotatua kero jaribuni kutumia mbinu tofauti" alisema.
Mhandisi Ndikilo alisema, kila mmoja anatakiwa kusimama katika nafasi yake kuhakikisha hakuna kero ambayo iko ndani ya uwezo wake na haijapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
" Wananchi leteni taarifa kama kuna mtumishi wa mkoa ambaye hawajibiki ipasavyo kwenye eneo lake, huu sio wakati wa kuendelea kuwavumilia watu ambao hawawajibiki katika nafasi zao" alisisitiza Ndikilo.
Katibu Tawala wa mkoa huo Dkt Delphine Magare alisema hatakuwa tayari kumvumilia mtendaji ambaye hatatekeleza ipasavyo majukumu yake na kwamba yeyote atakayeenda kinyume atamchukulia hatua za kinidham .
Awali akiongea katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo aliwataka watendaji kufanya kazi na kumsaidia Rais John Magufuli badala ya kuwa mzigo na kushindwa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.
" Wataalamu wafanye kazi zao mambo mengi wanaweza kuyamaliza kabla hayajafika mbali, wazitendee haki dhamana zao, wasilundike kero za wananchi na kugeuka kuwa mizigo kwa kushindwa kusimamia nafasi zao" alisema.
Katika mkutano huo wananchi wengi walilalamikia suala la fidia ambalo alielekeza idara husika kulitafutia ufumbuzi wa haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.