“Napenda kutoa Rai kwa Wakulima wote wa Korosho Mkoa Pwani, kuwa waende katika shamba darasa la Ruvu JKT kwa ajili ya kujifunza namna ya upandaji wa miche ya Korosho ya kisasa”.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa uzinduzi wa upandaji wa Mikorosho mipya ,uliofanyika katika shamba la Ruvu JKT mwanzoni mwa wiki hii.
Mhe. Ndikillo alisema kwamba Serikali ya awamu ya Tano imeamua kulifanya zao hili la Korosho kuwa ni mojawapo mazao ya bishara ya kimkakati hapa nchini kwani ni moja ya zao ambalo linaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.
Pia alisema kuwa Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania imetoa kilo 7,182 za mbegu bora za Korosho kwa Mkoa wa Pwani na kuzisambaza katika halmashauri zote , ambapo mbegu hizo zinakadiriwa kuzalisha miche bora 1,039,687 ya korosho ambayo imeanza kutolewa bure kwa wakulima .
Ndikilo aliwataka Viongozi wa Wilaya na Halmashauri kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa miche hiyo, na taarifa za wakulima waliokabidhiwa miche hiyo ya Korosho zihifadhiwe vizuri kwa ajili ya ufatiliaji.
Aidha amewataka maafisa Ugani wa Halmashauri watoke maofisini, na kwenda kwa Wakulima kwa ajili ya kutoa elimu na kanuni za kilimo bora cha Korosho.
Katika hatua nyingine Mhe Ndikilo alisema kuwa misimu mitatu iliyopita kulikuwa na mfumo ukusanyaji wa Korosho na kutunzwa na vyama vya msingi( AMCOS) katika maeneo ya Vijijini ambapo mfumo huu ulileta changamoto nyingi sana husuani katika ubora na uzito kati ya mauzo kwenye minada na utoaji wa korosho kwa mnunuzi.
“Ningependa kutumia Fursa hii kuwakumbusha na kuwatahadharisha Viongozi wa (AMCOS) kubadilika na kama hawatakuwa tayari kubadilika na kusimamia mfumo uliowekwa kulingana na sheria ni afadhali wajivue wenyewe uongozi na tutawachulia hatua kali za kisheria “alisema Ndikillo.
Aidha Mhe. Ndikillo ametoa wito kwa wawekezaji wa Viwanda kuwa waje wajenge Viwanda vya kubangua korosho na vya kutengeneza magunia ya kuhifadhia korosho hapa nchini ili kuepukana na adha ya kuagiza magunia kutoka nje.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.